Wednesday, January 11, 2012

Mzee Kipara hatunaye tena Duniani

Msanii Mkongwe katika tasnia ya Maigizo/Filamu hapa nchini, Fundi Saidi almaarufu kwa jina la kisanii Mzee Kipara (pichani) amefariki Dunia mapema leo asubuhi,mahali alipokuwa akiishi maeneo ya Kigogo Mbuyuni jijini Dar es Salaam.

Mzee kipara ambaye alizaliwa mnamo mwaka 1922,huko Bongoni mkoani Tabora,alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya miguu kukosa nguvu,alikuwa hawezi kusimama mwenyewe,sambamba na umri nao kuenda ulichangia kwa maradhi hayo na mengineyo,hali iliyomlazimu kutumia muda mwingi kitandani wakati mwingine alishindwa kutoka nje mpaka watu waliokuwa wakienda kumuona wafanye kumtoa nje kwa kubadirisha hali ya hewa.

Mzee Kipara alianza sanaa hiyo ya maigizo mnamo mwaka 1964 kwa kufanya kazi za mitaani na baadaye akachukuliwa na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) sasa TBC Taifa.

Akiwa na kituo hicho, aliigiza katika michezo mingi na nafasi zake kubwa zilikuwa zile zenye kuonyesha utemi, wengi huita ukorofi.

Mnamo Mwaka 1999 akiwa na wasanii wenzake akina Zena Dilip, Rasia Makuka, Marehemu Mzee Rajab Hatia ‘Mzee Pwagu’ na Mama Ambiliki walijiunga katika Kundi la Kaole ambalo lilikuwa likirusha maigizo yake katika Runinga ya ITV ambalo lilitoa wasanii wengi sana wa kizazi kipwa wakiwemo kina Kanumba,Ray,Swebe na wengine wengi.

Mzee Kipara anatarajiwa kuzikwa kesho (12/01/2012) majira ya saa kumi jioni.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI

-AMIN-.

No comments: