Thursday, January 19, 2012

RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZARAMBI RAMBI KWA SPIKA JUU YA KIFO CHA MBUNGE SUMARI

Rais Jakaya Kikwete
Rais JAKAYA KIKWETE amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge Mheshimiwa ANNE MAKINDA kufuatia kifo cha Mbunge Jimbo la Arumeru Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi-CCM-Marehemu JEREMIA SUMARI.


Taarifa ya Ikulu imesema Rais amesikitishwa na kuhuzunishwa na kifo hicho ambapo Mheshimiwa SUMARI alikuwa Kiongozi aliyewatumikia vema wananchi wa Jimbo lake na katika utumishi wake ikiwa ni pamoja na kuwahi kuwa Naibu Waziri wa Uchumi na Fedha.


Katika salamu zake za rambirambi Rais KIKWETE amesema wananchi wa Arumeru Mashariki wamepoteza kiongozi wa kutegemewa ambaye pia ameacha pengo kwa Taifa hivyo amewaomba wafiwa kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.


Kufuatia kifo hicho, Familia ya Marehemu imesema Marehemu SUMARI ataagwa keshokutwa jijini Dar es salaam ambapo Jumapili atasafirishwa tayari kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika Jumatatu ijayo kijijini kwake huko Akheri Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha.


Naibu Spika wa Bunge Mheshimiwa JOB NDUGAI amesema Marehemu SUMARI amefariki Dunia baada ya kulazwa kwa siku kadhaa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es salaam Kitengo Cha Mifupa-MOI akitokea nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu zaidi kutokana na kusumbuliwa na Kiharusi pamoja na Uvimbe kwenye Ubongo.


Msiba upo nyumbani kwa Marehemu huko Mbezi Beach katika Manispaa ya Kinondoni.


Mungu ailaze roho ya Marehemu SUMARI mahali pema peponi Amina

No comments: