Tuesday, January 10, 2012

WALIOFUTIWA MTIHANI KURUDIA TENA MWAKA…


Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillip Mulugo akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari Dar es Salaama kuhusu uamuzi wa Serikali wa kuwarudisha wanafunzi 9,629 waliofutiwa mtihani wao wa darasa la saba kufanya tena mtihani huo mwezi Septemba mwaka huu. (Picha na Fadhili Akida).

SERIKALI imesema wanafunzi 9,629 waliofutiwa matokeo yao ya mtihani wa darasa la saba mwaka jana kutokana na kufanya udanganyifu, watarudia mtihani huo Septemba.
Hata hivyo kati ya jumla ya watahiniwa 9,736 waliofutiwa matokeo yao na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kutokana na udanganyifu wa aina mbalimbali, 107 hawataruhusiwa kurudia

mtihani huo kwani matokeo yao yamefutwa moja kwa moja.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, N a i b u Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, alisema watakaorudia mtihani huo ni wale waliobainika kuwa na majibu yenye mfanano usio wa kawaida.
“Hawa 107 ambao hatujawaruhusu kurudia mtihani ni waliokutwa na majibu kwa kukamatwa ama na karatasi, rula au viatu vilivyoandikwa majibu, walioandikiwa majibu na waliokariri darasa. Ieleweke kuwa ruhusa ya kurudia mtihani inatolewa mwaka huu tu,” alisisitiza Mulugo.
Alizitaka halmashauri za wilaya kushirikiana na shule husika kuhakikisha wanafunzi hao hawatoki nje ya mfumo wa elimu, lakini pia wazazi kwa kushirikiana na shule nao wahakikishe
wanasajili watoto hao kwa ajili ya mtihani huo kabla ya Januari 30, ili taarifa zao zifike NECTA.

Alisema Serikali imechukua uamuzi wa kuruhusu wanafunzi hao kurudia mtihani baada ya kupokea malalamiko na maoni kutoka kwa wazazi, walezi, jamii na wadau wengine wa elimu.
Aliongeza kuwa wanafunzi watakaorudia mtihani wa Septemba, halmashauri na shule husika zitapaswa kuweka utaratibu wa ama kuingia madarasani na wenzao kusoma au kuwapa mafunzo ya jioni ili wamudu kufanya mtihani huo.
Aidha, alisema pamoja na ruhusa hiyo, pia imeundwa Tume ya Kuchunguza chanzo cha udanganyifu huo na kutoa mapendekezo ya kudhibiti udanganyifu kwenye mtihani.
“Tume hii imepewa miezi minne kufanya kazi hiyo na itawasilisha taarifa yake Aprili,” alisema

Naibu Waziri.
Alisema kuundwa kwa Tume hiyo hakutofuta hatua ambazo tayari zimeanza kuchukuliwa katika baadhi ya maeneo dhidi ya watakaobainika kuhusika na udanganyifu huo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa wizara hiyo itachukua hatua kali ili iwe fundisho dhidi ya watakaobainishwa na Tume kuhusika na udanganyifu huo, kwa kuwa kitendo hicho

kisipokemewa, kitalifikisha Taifa pabaya.
Aliwataka wazazi, walezi na jamii kwa jumla, kutambua kuwa jukumu la utoaji, usimamizi na uendeshaji wa elimu ni la wote, hivyo wajiepushe na udanganyifu kwenye mitihani na kulea watoto wao katika misingi ya maadili mema, kujiamini na kujitegemea katika maisha yao.
Hivi karibuni, NECTA wakati ikitoa matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka jana ilisema kati ya watahiniwa 983,545 waliofanya mtihani huo, 567,767 sawa na asilimia 58.28 walifaulu ambapo watahaniwa 9,736 walifutiwa matokeo baada ya kubainika udanganyifu katika mtihani huo.

No comments: