Thursday, January 19, 2012

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUZALISHA NISHATI YA KUNI NA MKAA

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Ezekieli Maige alipokuwa akiwaeleza wafanyakazi wa Msitu wa Hifadhi Ruvu uliopo Kibaha, Mkoani Pwani nia ya Wizara kuanza kuzalisha nishati ya mkaa na kuni, hivi karibuni.

Na Tulizo Kilaga

WIZARA ya Maliasili na Utalii iko kwenye mchakato wakuangalia uwezekano wakutumia maeneo yake yalioko Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya uzalisha wa nishati ya kuni na mkaa.

Hatua hiyo inakuja kufuatia kukosekana kwa ufumbuzi wa tatizo la nishati ya kuni na mkaa ambao kwa miaka yote asilimia kubwa ya nishati hizo hasa mkaa hutumika jijini Dar es Salaam.

Katika ziara yake ya kutembelea misitu ya hifadhi iliyoko Mkoani Pwani hivi karibuni, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Ezekiel Maige alisema kwa miaka yote asilimia karibia 50 ya nishati ya kuni na mkaa unaozalishwa nchini unatumika jijini Dar es Salaam kutokanawakazi wake kushindwa kutumia nishati nyingine kama umeme na gesi.

“Hali ilivyo sasa ni lazima tukubari tutaendelea kutumia mkaa kwa miaka kadhaa ijayo,na ili kufanya hivyo ni lazima tujipange kuwa wazalishaji wa mkaa, Wizara sasa haioni haja yakusubiri watu wachome mkaa na kuanza kukimbizana nao na badala yake imeamua kukabiliana na mahitaji ya nishati hiyo,” alisema Mhe. Maige.

Aliongeza kuwa kanuni ya uchumi zinasema kuwa jinsi unavyoongeza ugavi ndivyo unavyopunguza bei, na jinsi unavyopunguza bei ndivyo unavyowapunguzia hamu wazalishaji wapya kuingia kwenye eneo hilo kwa sababu halitakuwa na faida. Hivyo wizara inaweka mikakati yakuzalisha mkaa.

“Wizara kwa kupitia Wakala wake wa Huduma za Misitu (TFS) inafikilia kuanzisha mashamba ya kuni ambapo itapanda miti inayokomaa kwa muda mfupi na baadaye kuchoma mkaa na kufungua vituo vya kuuzia mkaa kwa bei nafuu kuliko mkaa wa wizi au mkaa unaotozwa ushuru mwingi kwenye maeneo yaiyoruhusiwa,” alisema Waziri.

Mhe. Maige alisema hatua hiyo itaiongezea kipato TFS na kuwapa changamoto wazalishaji wa nishati nyingine na kupunguza presha ya uvamizi wa misitu kwenye maeneo ambayo yamezuiwa.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa mpango huo utahusisha sekta binafsi kwa kuwa sheria inaruhusu kuingia mkataba wa muda mrefu na watu wanaotaka kuendeleza misitu. Hivyo wawekezaji hao watalazimika kupanda miti na kuuza huku ardhi ikibaki serikalini ili kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu, Bi. Monica A. Kagya alisema wakati wa kuanzisha mashamba hayo watazingatia mahitaji ya wakazi wa maeneo husika na kuchanganya aina ya miti kutokana na mahitaji ya wananchi, lakini dhumuni kuu litakuwa kupata kuni na mkaa.

Aliongeza kuwa, zoezi hilo litaanza kutekelezwa mara baada ya wataalamu wa misitu kukamilisha utafiti wa aina ya miti inayofaa kupandwa na kukomaa kwa muda mfupi huku ikizalisha mkaa mzito unaopendwa na wengi.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwamtumu Mahiza alisema atahakikisha vijana wanaotumia nguvu kazi zao kufanya uharibifu, wanashirikishwa kwa nguvu zote katika shughuli za upandaji miti inayokomaa kwa muda mfupi kuanzia msimu huu wa mvua ili kuweza kuzalisha nishati ya kuni na mkaa kwa wingi bila kusababisha uharibifu wa mazingira.

Mkoa wa Pwani ni eneo linaloathilika zaidi na mahitaji ya mazao ya misitu ya mkoa wa Dar es Salaam kutokana na ukaribu wa mikoa husika ambapo takwimu za mwaka 2010 zinaonyesha kuwa Tanzania hutumia magunia milioni 64 ya mkaa kwa mwaka ambapo nusu ya hayo hutumika jijini Dar es Salaam.

No comments: