Friday, January 20, 2012

Fisi ala mtoto wa mwaka mmoja

KATIKA kipindi kisichozidi wiki mbili, mtoto mwingine amenyakuliwa na fisi akiwa nyumbani kwao na mama yake na kukimbia nae vichakani, akamla na kutokomea vichakani. Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Diwani Athumani alisema jana kuwa, fisi huyo alimnyakuwa na kumla mtoto Happiness Makambi (1) juzi saa moja usiku katika Kijiji cha Kidinda, Tarafa ya Ntuzu wilayani Bariadi.
Kwa mujibu wa Kamanda Athumani, kabla ya mauaji hayo, mama mzazi wa mtoto huyo, alimweka nje mwanaye kwenye mkeka na kuingia ndani mara moja wakati akiwa katika harakati za upishi jikoni. Wakati mtoto Happiness akiwaanje na mama yake akiendelea na mapishi, fisi huyo alimng’ata mtoto Happiness shingoni na kutoweka naye porini. Mama Happiness alipiga kelele za kuomba msaada na wananchi kwa kushirikiana na ofisa wanyamapori na maofisa wa polisi walianza msako wa kumtafuta fisi huyo lakini juhudi zao hazikufanikiwa kumpata juzi hiyo. Msako huo uliendelea na kumpata fisi huyo jana akiwa amejificha kwenye shamba la mahindi ambapo alishambuliwa kwa kupigwa risasi na polisi na wananchi walisaidia wakitumia silaha mbali mbali za jadi. Kamanda Athumani alisema walipompasua tumboni fisi huyo, alikutwa akiwa na baadhi ya viungo vya binadamu ikiwa ni pamoja na fuvu na mguu wa kushoto wa mtoto Happiness aliyenyakuliwa na kuliwa na fisi juzi. Tukio hilo limetokea katika kipindi kisichozidi wiki mbili baada mtoto Wande Manjale (4) kunyakuliwa na fisi akiwa umbali wa meta 50 kutoka nyumbani kwao katika Kijiji cha Giriku Kata ya Bunamhala wilayani Bariadi. Hata hivyo fisi huyo alimtupa mtoto aliyemyakua baada ya kuona kundi kubwa la wananchi wenye silaha likimkimbiza na kutokomea porini ambako hakuonekana.

Habari Leo

No comments: