Thursday, February 16, 2012

CCM YAFAFANUA ZAIDI KUHUSU BARAZA LA USHAURI LA WA WASTAAFU

Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Nape Nnauye

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kumekuwa na tafsiri zisizosahihi juu ya baadhi ya maamuzi yaliyofanywa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichoketi mjini Dodoma tarehe 12/02/2012 chini ya uenyekiti wa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Jambo kubwa ambalo linapotoshwa sana ni la uamuzi wa NEC kuunda baraza la Ushauri la Wazee. Uamuzi ambao kimsingi ulifikiwa kwenye kikao cha NEC cha mwezi Aprili mwaka 2011 Mjini Dodoma kikao ambacho kiliridhia kufanyika kwa mageuzi ndani ya Chama.
Kikao cha tarehe 12/02/2012 cha NEC kiliridhia tu mabadiliko ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2010 ili kuruhusu kuundwa kwa baraza hilo.
MSINGI WA UAMUZI HUU.
#. Ni ushauri wa wastaafu wenyewe.
Wazo la kuundwa kwa baraza hili lilitokana na ushauri wa baadhi ya wazee wenyewe wastaafu wakizingatia wingi na urefu wa vikao husika, na si mpango au mkakati wa kuwaengua makusudi wastaafu hao kama inavyodaiwa na baadhi ya wapotoshaji.
Ilikuwa ni ushauri wao kwamba baada ya kustaafu badala ya kulazimika kuhudhuria vikao vya kitaifa kila mara basi wapewe muda wa kupumzika na wanapotakiwa kutoa ushauri watumiwe badala ya utaratibu wa sasa wa kulazimika kuhudhuria vikao ambavyo kwakweli ni vingi na wakati mwingine huisha usiku wa manane.
#. Umuhimu wa busara zao kwa Chama.
Baada ya wazo la wazee wetu kupumzika, huku tukizingatia kuwa busara zao bado ni muhimu sana kwa Chama na Taifa, busara ikatumika badala ya kupumzika kabisa basi tuunde Baraza la Ushauri la Viongozi wa Kitaifa wastaafu.
Na hii haina maana kuwa hawaruhusiwi kuhudhuria vikao vya Chama na kuwa hawatatumika kwa kazi za Chama na Taifa kwa ujumla, isipokuwa mabadiliko haya yanaondoa ulazima wa wao kuhudhuria vikao hivyo kama ilivyokuwa mwanzo.
#. Ni namna bora ya kuwaenzi kwa mchango wao kwa Chama.
Chama makini chochote kitatafuta utaratibu bora wa kuwaenzi waasisi wake na kuendelea kuvuna busara na hekima zao katika kuendelea kukijenga Chama. Katika hili CCM imeonyesha mfano mzuri unaostahili kuigwa na vyama vingine. Kuundwa kwa baraza hili na kutambuliwa rasmi na katiba ya Chama ni uthibitisho tosha wa namna CCM inavyothamini wastaafu hawa.
Kwa kuwaundia baraza la ushauri ni namna nzuri ya kuendelea kutumia busara zao kwa kutumia chombo kinachotambulika kikatiba.
Wajumbe wa baraza hili.
Kwa mujibu wa uamuzi huo wajumbe wa baraza hili ni:
1. Wenyeviti wastaafu wa CCM Taifa ambao kwa utamaduni wa CCM huwa pia ndio Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. Makamu wenyeviti wastaafu bara na visiwani, ambapo kwa Zanzibar kwa mujibu wa utamaduni wa CCM ndio huwa pia marais wastaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mwenyekiti wa baraza hili atakuwa ni Mwenyekiti yule aliyewatangulia wenzake kustaafu. (seniority). Na watakutana pale tu wanapoona ipo haja ya kukutana.
Wanaweza kuombwa kuhudhuria vikao vya Kitaifa au wao kuomba kuhudhuria kulingana na mazingira na mahitaji ya wakati husika.
Kazi kubwa ya baraza hili ni kushauri Chama na serikali zake zinazotokana na CCM na si kudhibiti Chama, Serikali na Viongozi kama inavyotafisiriwa na baadhi ya wapotoshaji.
CCM inawasihi wale wanaoendelea kupotosha maamuzi haya kwa makusudi au kwa bahati mbaya kuacha mara moja upotoshaji huo, kwani una lengo la kuonyesha kuna mgogoro mkubwa kati ya Chama na wazee wetu wastaafu wakati ukweli si huo.
Chama Cha Mapinduzi kinathamini sana busara na mchango wa wastaafu hawa katika ujenzi wa Chama na Taifa kwa ujumla hakiwezi kuwaong'oa au kuwatupa kama inavyojaribu kupotoshwa na baadhi ya watu. Tuwatendee haki wazee wetu hawa badala ya kutumia majina yao na uamuzi wa Chama ambao una baraka zao vibaya.
Imetolewa na:-
Nape Moses Nnauye
KATIBU WA NEC ITIKADI NA UENEZI CCM TAIFA
15/2/2012

No comments: