Wednesday, February 29, 2012

Chilligati atishia kujiuzulu sekretarieti CCM


Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Chiligati
Ramadhan Semtawa
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Chiligati juzi alitaka kujiuzulu ujumbe wa Sekretarieti ya chama hicho mbele ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kutokana na kukerwa na kile alichokiita kuvuja kwa siri za kikao cha sekretarieti hiyo iliyoketi mwishoni mwa wiki kujadili mchakato wa kura za maoni kuelekea uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki.


Kikao hicho cha Sekretarieti kilichoketi Dar es Salaam, kilikotoka na pendekezo la kutaka mshindi wa kura za maoni Sioi Sumari atoswe kutokana na sababu kuu mbili, utata wa uraia wake kutokana na kuzaliwa Kenya na kutoungwa mkono na wagombea wenzake.


Sekretarieti hiyo ambayo ilitoa mapendekezo hayo kwa Kamati Kuu (CC) ya CCM, pia ilitoa angalizo kwamba kama Sioi angepitishwa, chama kingekuwa katika hatari ya kuwekewa pingamizi kutokana na madai hayo ya utata wa uraia na pia, vigogo wengine wangekisaidia Chadema ili kishinde uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Aprili Mosi, mwaka huu.


Siku iliyofuta mkakati huo ulivuja katika vyombo vya habari siku ambayo pia kulikuwa na kikao cha CC na ndipo Chiligati alipolalamika mbele ya Mwenyekiti Kikwete akidaiwa kusema: “Haiwezekani mambo tuliyojadili jana (siku ya kikao) yaandikwe katika magazeti neno kwa neno.”


Alipoulizwa jana kuhusu tishio lake la kutaka kujiuzulu Chiligati alisema: “Mambo ya Ngoswe mwachie Ngoswe mwenyewe.” Mahojiano yake na mwandishi wetu yalikuwa kama ifuatavyo:


Swali: Salaam ndugu Chiligati. Kwanza heri ya mwaka mpya.
Jibu: Nzuri, nashukuru na wewe pia.


Swali: Nimesikia kuwa juzi ulitaka kujiuzulu ujumbe wa sekretarieti kutokana na kuvuja siri za kikao chenu cha juzi cha mchakato wa kura za maoni wa Arumeru Mashariki je, msimamo wako ukoje hadi sasa hivi?
Jibu: Bwana wewee! Sikia, hayo ni mambo ya ndani ya vikao. Mambo ya ngoswe mwachie ngoswe mwenyewe!


Swali: Sawa, natambua ni la vikao vya ndani vya chama, lakini huoni kuvuja kwa siri za vikao vyenu kunaonyesha sekretarieti imegawanyika?
Jibu: Nakwambia hivi, hayo ni mambo ya ndani ya vikao. Kwani wewe mbona hutuambii mambo ya nyumbani kwako na mkeo?


Swali: Hujaniuliza, ungeniuliza ningekwambia. Lakini, je, sasa kama siri zitaendelea kuvuja msimamo wako utakuwa ni upi?
Jibu: Haaah...! Wewe bwana shughulika na ya kwako, haya hayakuhusu. Haya ni sawa na mambo ya ndani ya nyumba, ni yetu wenyewe tutayazungumza kwenye vikao vyetu.


Swali: Lakini, tayari mmeweza kubaini ni vipi siri za vikao vyenu zinavuja na labda mmejua ni nani anayezivujisha?
Jibu: Nasema tuachie wenyewe, hatutaki utuingilie. Nasisitiza tena kitu kimoja, hilo halikuhusu endelea na mambo yako.


Wakati Chiligati akijibu hayo, taarifa kutoka ndani ya kikao hicho cha CC, zilisema kwamba baadaye Rais Kikwete aliitaka sekretarieti hiyo yenye watu tisa ijiangalie yenyewe kujua nani anavijisha taarifa za vikao.


Katika kikao hicho sekretarieti, mbali ya kumwekea vikwazo Sioi, kilitaka Sarakikya ambaye alishika nafasi ya pili apitishwe na chama.
Mkutano Mkuu wa jimbo hilo uliofanyika Februari 20 ulimchagua Sioi, mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Jeremiah Sumari kwa kura 361, akifuatiwa na William Sarakikya aliyepata kura 259, Elishilia Kaaya (176), Elirehema Kaaya (205), Anthony Musari (22) na Moses Urio (11).

Mwananchi

No comments: