Tuesday, February 7, 2012

Madaktari Bingwa Hospitali Ya Taifa Ya Muhimbili Sasa Watangaza Mgomo Rasmi

Wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii ikiwa aktika siku ya tatu ya kuzungumza na madaktari walio kwenye mgomo, madaktari mabingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na walio katika Taasisi ya Mifupa (MOI) waliokuwa wakiendelea na kazi, wameanza mgomo rasmi ili kuishinikiza Serikali isikilize madai yao haraka.



Akizungumza kwa niaba ya madaktari hao, Dkt.Catherine Mg'ong'o, ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya madaktari bingwa watano waliochaguliwa wiki iliyopita kwenda kuonana na Waziri Mkuu, Bw.Mizengo Pinda, alisema hawatafanya kazi hadi Serikali itakaposikiliza madai yao.



“Mgomo umeanza rasmi leo (jana), hatutafanya kazi hadi madai yetu yatakaposikilizwa, huduma zitasimama hadi tupate haki yetu kwani Serikali inafanya mzaha,” alisema.



Mgomo huo wa jana ulihusisha vitengo vyote huku wagonjwa waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo wakipewa taarifa za kuondoka katika wodi walimolazwa.



Azimio la mgomo huo lilifikiwa katika kikao cha dharura kilichoitishwa na jopo la madaktari bingwa wakiongozwa na Dkt. James Rwehabura ambaye ni daktari bingwa wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu.



Kutokana na azimio hilo, baadhi ya madaktari hao walionekana wakiingia katika magari yao na kuondoka huku wagonjwa wakiwa wameshika tama.



Habari za ndani kutoka katika kikao cha dharura cha wanataaluma hao, zilisema uamuzi huo ulifikiwa kwenye kikao cha madaktari hao kilichoanza mapema asubuhi jana na kumalizika saa 6:00 mchana. “Kwa pamoja tumekubaliana kuweka vifaa chini, hii ni kutokana na ukweli kuwa hali ya utoaji huduma katika hospitali hii ni mbaya huku taarifa za Serikali zikiwa siyo za kweli,” alidokeza mmoja wa madaktari bingwa.



Daktari huyo aliyekataa kutaja jina lake, alisema, “Tumekubaliana kugoma hadi hapo Serikali itakapotoa majibu ya madai yote yaliyowasilishwa na jumuiya ya madaktari inayoongozwa na Dkt Stephen Ulimboka kwa Serikali.” Jumuiya hiyo iliwasilisha madai mbalimbali likiwamo la kuitaka Serikali kupeleka vifaa na dawa katika hospitali za Serikali ili madaktari hao waweze kutoa huduma bora kwa jamii.



Pia, madaktari hao walitaka kusitisha safari za vigogo kwenda kutibiwa nje kwa magonjwa yanayotibika ndani kwa kile walichodai, hali hiyo inachangia wao kudharauliwa na pia kuzorotesha jitihada za Serikali katika uboreshaji wa mazingira ya kazi kwa madaktari hao.



Kwa nyakati tofauti, madaktari hao walibainisha sababu ya mgomo wao na kudai kuwa, kikubwa ni mazingira magumu ya kazi. Daktari mwingine ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini alisema, licha ya mishahara na posho ndogo, lakini mazingira ya kufanyia kazi yamekuwa magumu mno.



“Tumeshaamua, ‘tools down’ hospitali haina kitu, hata ‘mask’ hakuna badala yake tunavaa gozi tunapofanya upasuaji, acha hiyo, hata nyuzi za kushonea wakati wa upasuaji hakuna,” alisema daktari huyo. Daktari huyo alisema, hawawezi kufanya kazi katika mazingira hayo kwa sababu yatawasababisha kuwa na utendaji mbovu na baadaye taifa kuwalalamikia.



Alisema hapa nchini madaktari bingwa ni wachache, kwa hiyo kitendo cha wao kufanya kazi peke yao bila wasaidizi, yaani madaktari wa mafunzo na wale wanaomaliza, wanaelemewa na mzigo wa kazi.



Mgomo huo ulisababisha hali ya matibabu hospitalini hapo kudorora na kuwaacha madaktari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wasijue la kufanya.



“Kimsingi madaktari bingwa wametupa ushirikiano mkubwa sasa kutokana na mgomo huu, hatujui nini cha kufanya,” alisikika akisema mmoja wa madaktari wa JWTZ.



Dkt. Henry Mwakyoma, Mhadhiri Mkuu wa Chuo cha Udaktari Muhimbili, (MUHAS) ambaye hakuwapo katika kikao hicho cha dharura alidai kuwa, yeye kama mhadhiri hajagoma, lakini alikiri kuwapo kwa mazingira magumu ya kazi.



“Mpaka sasa hatujalipwa mishahara ya mwezi uliopita, halafu kazi yetu ndiyo kama hii tunatakiwa tufanye utafiti, unategemea tutafanya kazi kwa umakini kweli? Tutawafundisha madaktari kwa umakini?” alihoji Dkt. Mwakyoma.



Mwakyoma alisema, Serikali haiwezi kudai kuwa haina fedha za kutosha wakati imetumia mamilioni ya shilingi katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru na uchaguzi wa Igunga. Alisema ni vyema Serikali ikajipanga na kuamua kushughulikia masuala ya madaktari kwa hekima kwani kukaa kimya bila kutoa suluhu ni sawa na kufanya ushindani usio na maana.



Hata hivyo, Ofisa Habari Mwandamizi wa MNH Aminael Aligaesha alisema jana jambo hilo lilikuwa likishughulikiwa kwani vipo vikao vinavyoendelea.



No comments: