Wednesday, February 1, 2012

Maharamia wachoma moto boti ya uvuvi Tanga

Mkuu wa mkoa wa Tanga, Luteni (Mstaafu) Chiku Gallawa (mwenye kilemba) akimwagiza Mkuu wa wilaya ya Muheza Bw. Methew Nasei (kushoto) kufuatilia watu waliochoma moto boti ya doria ya uvuvi katika kijiji cha Kigombe wilayani humo baada ya watu wasijulikana kuichoma moto.
Mkuu wa mkoa akiwa na viongozi wa kijiji na wilaya ya Muheza wakiitazama boti ya hifadhi ya bahari ya Silikanti iliyopo Kigombe wilayani Muheza ambayo maharamia wa uvuvi wameichoma moto hivi karibuni kutokana na hifadhi hiyo kuendesha doria inayowakamata wavuvi haramu.
wananchi wa kijiji cha Kigombe na viongozi wa wilaya ya Muheza wakimskiliza Mkuu wa mkoa wa Tanga (hayupo pichani) alipofika kwenye kijiji hicho kukagua boti iliyochomwa na maharamia pamoja na mambo mengine mkuu huyo wa mkoa aliwataka wananchi kjulinda mazingira yao na waepuke uvuvi haramu.

Na Mashaka Mhando,Muheza

MAHARAMIA wanaoendesha uvuvi haramu katika mwambao wa bahari ya Hindi mkoani Tanga, wameichoma moto boti ya doria inayomilikiwa na Taasisi ya Hifadhi ya bahari ya Silikanti iliyopo katika kijiji cha Kigombe wilayani hapa.

Kuchomwa kwa boti hiyo iliyokuwa ikielea baharini katika eneo hilo la Kigombe, kunatokana na dori ya mara kwa mara inayofanywa na taasisi hiyo kwa ajili ya kuwasaka maharamia wanaoendesha uvuvi haramu wa kutumia mabomu na nyavu ndogo zisizoruhusiwa, kumeelezwa kwamba ndiko kuliwapa hasira maharamia hao, wakachukua maamuzi hayo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kigombe Bew. Mwambi Haji alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni (Mstaafu) Chiku Gallawa aliyefika katika kijiji hicho kupata maelezo ya kuchomwa kwa boti hiyo, alisema tukio hilo lilitokea hivi karibuni na hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Mhifadhi wa bahari ya Silikanti Bw. Sylevester Kazimoto alisema katika kipindi cha mwaka uliopita waliendesha doria 192 za baharini na nchi kavu iliyohusisha vyombo vya dola ambayo iliwezesha kukamatwa kwa wavuvi haramu wapatao sita.

Alisema pamoja na kuwakamata wavuvi hao pia walikamata vifaa vinavyotumika kwa uvuvi huo ikiwemo baruti 29, bunduki 17 za kuulia samaki, mitungi 31 ya kuzamia, makokoro 94, nyavu za utale 11 na samaki wa baruti kilo 124.

Akizungumza katika mkutano na wananchi waliofika katika ofisi ya hifadhi hiyo Mkuu wa Mkoa alisema kuwa kila wananchi analojukumu kubwa la kulinda na kuhifadhi rasilimali za bahari hivyo akawataka wataalamu wa hifadhi hiyo wakishirikiana na serikali ya kijiji kuandaa mpango wa kuorodhesha wavuvi wote na boti zao kisha kuziandika namba.

Alisema suala la uvuvi haramu hivi sasa linatakiwa kupigwa vita baada ya muda mrefu nchi yetu kuliacha bila kuwachukulia hatua watu wanaoendesha uvuvi haramu ambao licha ya kuharibu mazingira pia wanaleta matatiz ya kiafya kwa kuvua samaki wa aina hiyo.

Hata hivyo, mjumbe wa serikali ya kijiji hicho Bw. Hassain Bakari almtaka mkuu huyo wa mkoa kuingilia kati suala la wavuvi haramu kukamatwa kisha kesi zao kuishia hewani kwa maana ya polisi na mahakamani hatua ambayo inasababisha wavuvi hao kutawala mwambao wa bahari kwa kuendesha vitendo hivyo wakiamini kwamba, wakikamatwa kesi zao watazimaliza.
Habari kwa Hisani ya Issa Michuzi Blog

No comments: