Monday, February 13, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AENDELEZA KAMPENI YA USAFI WA MAZINGIRA MKOANI HUMO

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya akihamasisha usafi wa mazingira kwa wafanyabiashara wadogowadogo wanaoendesha shughuli zao katika soko dogo la majengo Mkoani humo. Hatua hiyo ni sehemu ya kampeni ya kudumu ya Usafi wa mazingira katika Mji wa Sumbawanga ambayo inashirikisha taasisi na wananchi wote katika kuhakikisha Mji wa Sumbawanga unakuwa safi. Kampeni hiyo ilianzishwa na uongozi wa Mkoa wa Rukwa ukiongozwa na Mkuu huyo wa Mkoa tarehe 12 Januari 2012 iliyokuwa siku ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kampeni hiyo itazinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Billal ambaye atakuwa Mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi ya siku 7 kuanzia tarehe 18-24 Februari 2012.
Mkuu wa Mkoa aliendelea na uhamasishaji kwa wafanyabiashara wanaochoma mahindi katika maeneo ya kata ya Majengo katika Manispaa hiyo. Aliwaasa wafanyabiashara hao kuheshimu sheria kwa kuhakikisha maeneo ya biashara yao yanakuwa safi kuepuka magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu. Aliwaomba wafanyabiashara wote wamuunge mkono katika kampeni hiyo ili Mji wa Sumbawanga uweze kufanya mapinduzi katika usafi wa mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alihamasika kuona mkusanyiko mkubwa wa watoto ambao walitoka kwenye mafundisho ya komunio ya kwanza katika kanisa la Kristo Mfalme na kuamua kuongea nao. Alitumia fursa hiyo kuwahamasisha kuchukia uchafu na hivyo kuwa mstari wa mbele katika kupenda usafi kwa kufanya usafi majumbani mwao, mashuleni na hata nje ya maeneo hayo. Wanafunzi hao walifurahi kuongea na Mkuu wa huyo wa Mkoa na kuahidi kushiriki katika usafi wa mazingira.

No comments: