Saturday, February 11, 2012

Wabunge watakiwa kuangalia maslahi ya nchi katika mchakato wa katiba mpya

Na Mwandishi Wetu,Dar es salaam.

WAKATI mjadala wa Mabadiriko ya Sheria ya Katiba Mpya ukiendelea Bungeni,baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini wamewataka Wabunge kuacha kuwahadaa wananchi kwa kuyumbisha mchakato wa katiba mpya na badala yake waweke mbele maslahi ya Taifa.

Viongozi hao walitoa kauli hiyo kufuatia misuguano iliyopo baina ya wabunge wa Chama tawala CCM kwa upande mmoja na CHADEMA kwa upande mwingine kuhusu Mabadiliko ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba mpya yaliwasilishwa bungeni na Serikali.

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia yeye alisema mchakato wa marekebisho ya sheria hiyo lazima umalizike kwa wakati ili kutoa nafasi kwa utekelezaji wa sheria hiyo.

Alisema kuwa, malumbano yanayoendelea ndani ya Bunge yanahatarisha mustakabali wa utekelezaji wa sheria hiyo kwa wakati.

Mwenyekiti wa chama cha UPDP Fahamy Dovutwa yeye alisema, wabunge waweke maslahi ya taifa mbele badala ya kuangalia itikadi zao huku Peter Kuga Mziray wa APPT Maendeleo akiwataka wabunge wa CCM kuunga mkono mabadiliko hayo ili mchakato huo uanze.

Hata hivyo baada ya malumbano ya siku mbili, wabunge walipisha mabadiliko ya sheria ya uundwaji wa tume ya kuratibu maoni ya wananchi kuhusu uandikwaji wa katiba mpya.

Kufuatia hatua hiyo sasa Rais Jakaya Kikwete anaweza kuunda tume hiyo, ambayo itakuwa na kazi ya kuratibu maoni ya wananchi kuhusu uandikwaji wa katiba hiyo.

No comments: