Saturday, February 11, 2012

WANAHARAKATI WATOA TAMKO KUHUSU KUMALIZIKA KWA MGOGORO KATI YA SERIKALI NA MADAKTARI 10.02.2012











Sisi
wanaharakati wa haki za binadamu,baada ya kuzingatia kwa kina
matukio,maamuzi na matokeo yaliyojiri kwa kipindi cha takribani wiki
tatu (Kuanzia Tarehe 21 Januari hadi 9 Februari 2012) za mgogoro kati
ya madaktari nchini tumebaini;









1.KUWA,
mgogoro huu umevunja haki ya kuishi kwa wananchi kadhaa na
umehatarisha haki za raia wengi sana; inakadiriwa kuwa wananchi wengi
wamekufa kwa kipindi hiki cha mgogoro huku wengi zaidi wakipata madhara
yasiyorekebishika na huku maelfu wakiteseka na maumivu makali;









2.KUWA,
Serikali imeonesha udhaifu mkubwa katika kutumia mamlaka iliyopewa na
wananchi ,hususani wajibu wake wa kusimamia haki za binadamu;ikiwa ni
pamoja na kutotoa maamuzi sahihi na kwa wakati na hivyo kusababisha
madhara makubwa kwa jamii;









3.KUWA,
Serikali imeshindwa kutumia rasilimali tulizoikabidhi, kutatua tatizo
hili huku ikifumbia macho matumizi mabaya na makubwa ya fedha za umma
ya
maafisa na viongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Aidha
viongozi wa Wizara hii wameshindwa kabisa kutoa uongozi stahiki kwa
watendaji na madaktari ambao ndio watekelezaji na watoa huduma kwa
jamii.









4.
KUWA, Katiba inatoa jukumu la moja kwa moja kwa wananchi kuchukuwa
hatua za kuiwajibisha Serikali kutekeleza wajibu wake;na kwamba,pale
wananchi tulipochukua jukumu la kuikumbusha Serikali wajibu wake na
kuitaka kuchukuwa hatua stahiki na za haraka kutatua matatizo haya,
Serikali imechukuwa uamuzi wa kutumia mabavu kutukamata na
kututisha.Siyo tu kuwa hii haikubaliki lakini pia ni ukiukwaji wa haki
za binadamu na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.









5.KUWA,
majibu yaliyotolewa na Serikali kama hatua za kutatua mgogoro
yameonyesha ishara ya nia njema ingawa yanahitaji utekelezaji wa
kuaminika;




pia
tumebaini kuwa kinyume cha katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania,
kumekuwa na utamaduni wa uongozi wa juu kutowajibisha na kutowajibika
kwa vitendo viovu kama hivi : Kwa maaana hii, kutokumwajibisha na
kuwajibika kwa Waziri wa Afya na Naibu wake ni kinyume na kanuni za
uwajibikaji na kulindana.









6.KUWA,
Bunge ambalo ndilo msimamizi wa Serikali, halikuchukuwa hatua za haraka
kuiwajibisha Serikali na kwa kuwa mwenendo wa Spika na Naibu Spika
umejikita katika ufinyu wa kutafsiri kanuni kwa ajili ya maslahi ya
umma na uhai wa Watanzania;









7.Na KUWA,Ibara ya 26 ya Katiba Ninamtaka kila raia wa nchi hii kuilinda Katiba na sheria zingine za Nchi;









HIVYO
BASI; Tunawasihi wananchi wenzetu kuwa,ni vema sasa tuchukue nafasi
yetu kuitaka Serikali kuwajibika kwa madhara yaliyotokea,kuikumbusha haja ya kuchukuwa hatua za ziada kurejesha hali ya kawaida kwenye hospitali za umma na kutekeleza ahadi zake kwa madaktari ;









1.
Tunawataka Waziri wa Afya Haji Mponda na Naibu Waziri Lucy Nkya
wajiuzulu mara moja kwa kushindwa kutatua mgogoro huu wa madaktari na
kusababisha vifo na madhara makubwa kwa Watanzania. Ama sivyo tunamtaka
Rais Jakaya Mrisho Kikwete awafukuze kazi haraka iwezekanavyo.









2.
Waziri Mkuu autangazie umma,ndani ya wiki moja ni hasara gani, ni
madhara kiasi gani ambayo Wananchi na Taifa limepata kwa kuingia kwenye
mgogoro na madaktari.









3.
Spika wa Bunge,auombe radhi umma juu ya hatua na kauli zake za kibabe
Bungeni kuzima hoja za Wabunge kutafakari mgogoro huu huku akijua kuwa
kwa kufanya hivyo ni kuendeleza maafa yaliyokuwa yanayowakumba
watanzania.









4.
Tume iliyounda kushughulikia tatizo hili itoe taarifa zake kwa umma
kila mwezi ili wananchi waweze kufuatilia utekelezaji wa makubaliano.









5.
Kutokana na mgogoro huu wa madaktari Serikali ijifunze kuchukuwa hatua
mara moja kila linapotokea tatizo ili kuepusha madhara yeyote.









6.
Tunawashukuru madaktari kwa kurudi kazini leo na tumetembelea
hospitali zote za umma Mkoani Dar es salaam na tumeshuhudia huduma za
tiba zikiendelea. Tunawaomba sana muendelee kuwahudumia wananchi kwa
moyo wote na linapotokea tatizo meza ya majadiliano itumike ili kuepusha
madhara kama tulivyoshuhudia kwenye mgogoro huu.









7.Mamlaka
zote nchini zitambue,ziheshimu na kuwajibika kwa wananchi walioziweka
madarakani kwa mujibu wa Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.









Pia
ni vema tukakumbuka kuwa nchini duniani zimekuwa na tabia ya
kuwashikilia, kuwashitaki na kuwatishia watetezi wa haki za binadamu
kwa tuhuma zisizo na msingi ili kuendeleza unyanyasaji na ukandamizaji.
Serikali itambue kuwa pale Serikali zilipokuwa zikijikita kwenye tabia
hizi kandamizi, ziliambulia kuongeza matatizo na hata kuishia kumwaga
damu za watu wake na hata viongozi wenyewe. Wanaharakati tunaomba
mshikamano na umoja kutoka kwa wananchi wote wenye uchungu na mapenzi
mema kwa taifa letu.







Imetolewa na:



Policy Forum, TGNP, LHRC, SIKIKA, TAMWA, HAKIARDHI, HAKIELIMU, GDSS, Jipange, ForDia na FemAct.

No comments: