Wednesday, March 21, 2012

BARAZA LA KISHWAHILI TANZANIA LAMPONGEZA MBUNGE KIGOLA KWA KUKATAA WAWEKEZAJI WASIOJUA KISHWAHILI


YAH: KUMPONGEZA MBUNGE KWA KUWAKATAA WAWEKEZAJI WASIOJUA KISWAHILI JIMBONI MWAKE

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) linampongeza Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, Mhe. Mendrady Kigola kwa kuishauri serikali kutowaruhusu wawekezaji wasiojua Lugha ya Kiswahili kuwekeza jimboni mwake.

Mhe. Kigola ameeleza sababu iliyomfanya afikie uamuzi huo kuwa ni kuzuia utapeli unaofanywa na baadhi ya wawekezaji kuingia mikataba batili na wananchi wasiojua lugha za Kigeni.

Kauli ambayo iliungwa mkono na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Ezekiel Maige na kutoa ushauri kuwa wawekezaji hao watafutiwe fursa ya mafunzo ya muda mfupi ya lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo lugha ya Taifa letu.

BAKITA kwa kutambua mchango huo linatoa pongezi hizi kwa wadau wote wa Kiswahili wanaosisitiza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili, kwani wazalendo hawa wanaendelea kutekeleza baadhi ya matamko mbalimbali yanayosisitiza matumizi ya Kiswahili likiwamo tamko la Mei 2005, la aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Mhe. William Lukuvi.

Mheshimiwa Lukuvi aliagiza taarifa za mikutano, semina na warsha nchini zitolewe kwa Kiswahili. Pia taarifa za miradi inayohusu wananchi ni lazima zitolewe kwa Lugha ya Kiswahili, ikiwa ni pamoja na vipeperushi na nyaraka zinazohusu miradi hiyo.

Imeandaliwa na: Richard P. Mtambi
​ Kaimu Katibu Mtendaji,
​ Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)
​ DAR ES SALAAM.


No comments: