Friday, March 16, 2012

NEC Yatuta Rufaa Chadema


Thursday, 15 March 2012 20:07
Neville Meena na Mussa Juma, Arumeru
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetupilia mbali rufaa ya Chadema dhidi ya mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki.

Joshua Nassari ambaye ni mgombea wa Chadema alikata rufaa NEC akitaka kutenguliwa kwa uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Arumeru Mashariki ambao ulitupilia mbali pingamizi lililokuwa likitaka mgombea wa CCM, Sioi Sumari aondolewe kwenye uchaguzi huo.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Mallaba alisema eneo la Usa River jana kuwa baada ya kupitia rufani ya Chadema, NEC imekubaliana na uamuzi uliotolewa awali na msimamizi wa uchaguzi.

“Msingi wa pingamizi hadi kukatwa kwa rufani ni suala la uraia wa mgombea wa CCM, na tume (NEC) imelifanyia kazi suala hili kwa kupitia sheria ya uraia namba 6 ya mwaka 1995 na kubaini kwamba Sioi Sumari ni raia wa Tanzania kwa kurithi,”alisema Mallaba na kuongeza:

“Ni kweli kwamba Sioi alizaliwa Thika nchini Kenya mwaka Mei 11, mwaka 1979, lakini wakati wazazi wake wote wawili ni raia wa Tanzania, na kwa sheria hiyo mtu anapata uraia ikiwa wazazi wake wote ni raia”.
Mallaba alisema kutokana na sheria hiyo, Sioi hakulazimika kuukana uraia wa Kenya ambao hakuwahi kuwa nao, kwani ni raia wa Tanzania.

Mkurugenzi huyo uchaguzi alisema kwa kuzingatia asili ya malalamiko ya Chadema walifanya marejeo kwenye Ibara ya 89 ya Katiba ya zamani ya Kenya ambayo walibaini kwamba ili mtu apate uraia wa nchi hiyo ni lazima mmoja wa wazazi wake awe raia wa nchi hiyo. “Uraia wa wazazi wa Sioi halikuwa na ubishi kwani hata wa rufani hawakulieleza, hivyo kwakuwa wazazi hao hakuna hata mmoja aliyekuwa na uraia wa Kenya,basi tume iliridhika kwamba mgombea huyo ni raia wa Tanzania,”alisema Mallaba.

Mallaba alisema Nassari katika rufaa yake alishindwa kuweka vielelezo vyovyote vinavyothibisha kwamba Sioi aliwahi kuwa raia wa Kenya na badala yake alijikita kwenye hoja moja tu kwamba mgombea huyo wa CCM alizaliwa Kenya.

Taarifa rasmi ya NEC kuhusu uamuzi huo iliyotolewa kwa waandishi wa habari jana inasema katika moja ya sehemu zake: “Katika maelezo ya mrufani (Nassari) hakuna popote ilipothibitishwa kuwa mrufaniwa (Sioi) alipata uraia wa Kenya”.Soma zaidi www.mwananchi.co.tz

No comments: