Sunday, April 8, 2012

CHADEMA Kugombea Ubunge Afrika MasharikiChama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinatoa taarifa kwa umma kwamba uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea ujumbe wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kupitia CHADEMA umekamilika tarehe 6 Aprili 2012 saa 10 Jioni.

Uteuzi wa mwisho wa wagombea utafanyika tarehe 9 Aprili 2012 siku ya jumatatu kuanzia saa 3 asubuhi ambapo wagombea wote waliorudisha fomu wametaarifiwa kufika kwenye mkutano husika.
Wagombea waliorudisha fomu mpaka sasa ni pamoja na Godfrey Mnubi, Edgar William Chibura, John Simon Malanilo, Patrick Lubango Nkandi, Anna E. Maghwira, Deogratias George Assey, Pasquina Ferdinand Lucas, Deusdedit Jovin Kahangwa, Antony Calist Komu na Mwantum Khamis Mgonja.
Ikumbukwe kuwa tarehe 12 Machi 2012 Katibu wa Bunge alitoa Taarifa kwa Umma kwamba, Uchaguzi wa wajumbe tisa (9) watakaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki utafanywa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wakati wa Mkutano wake wa Saba utakaofanyika Dodoma, kuanzia tarehe 10 hadi 20 Aprili, 2012.
Uchaguzi huo wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki unafanyika kwa kuzingatia kuwa maisha ya Bunge hilo lililoingia madarakani mwaka 2006 yatafikia ukomo wake 04 Juni, 2012.

Taarifa imetolewa kwa vyombo vya habari na:
John Mnyika
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
07/04/2012

No comments: