Friday, April 6, 2012

HOTUBA YA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MH. EZEKIEL MAIGE (MB) KATIKA UZINDUZI WA BODI YA WAKURUGENZI YA BODI YA UTALII TANZANIA (TTB)



Mhe.Ezekiel Maige
Ndugu Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Charles A. Sanga;
Ndugu Wakurugenzi wa Bodi;
Ndugu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii;
Menejimenti ya Bodi ya Utalii;
Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana;
Ni furaha kubwa kwangu kujumuika nanyi leo katika uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania. Napenda kuchukua fursa hii kukupongeza Balozi Charles Sanga kwa kuteuliwa kwako na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania ambacho ni chombo muhimu sana katika maendeleo ya sekta ya utalii hapa nchini. Uteuzi huu ni uthibitisho wa imani kubwa aliyonayo Mh. Rais kwako. Aidha nawapongezeni pia Wakurugenzi wote mlioteuliwa kuongoza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Hongereni sana!
Ndugu Mwenyekiti,
Kama mnavyofahamu utalii ni moja ya sekta ambazo ni mhimili mkuu wa uchumi ya nchi yetu hivi sasa. Serikali imekusudia kuendeleza sekta hii ili iongeze mchango wake kwenye pato la taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Tangu kuundwa kwa Bodi ya Utalii takriban miaka 18 iliyopita, imeweza kuchangia kuleta mafanikio makubwa katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini. Mifano michache ya mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la mapato yanayotokana na utalii kutoka dola za kimarekani milioni 146.84 mwaka 1993, hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 1.3 mwaka 2010. Aidha idadi ya watalii imeongezeka kutoka 230,166 mwaka 1993 hadi kufikia watalii 867,994 mwaka 2011. Haya ni baadhi tu ya matunda ya kazi nzuri inayofanywa na Bodi ya Utalii Tanzania, sambamba na taasisi nyingine za umma na binafsi. Napenda kuchukua nafasi hii Kwa niaba ya serikali kuipongeza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa kazi nzuri inayofanya ya kuitangaza Tanzania kama moja ya nchi zenye vivutio vikubwa na vya pekee barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Ndugu Mwenyekiti,
Serikali itaendelea kutoa kipaumbe katika kuhudumia sekta hii, ikiwa ni pamoja na kujenga miundo mbinu, kuongeza bajeti ya utangazaji, kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji, kuboresha huduma kwa watalii kama vile malazi, chakula, usafiri na kadhalika. Nataka nisisitize kuwa ubora wa huduma kwa watalii sambamba na kuimarika kwa utangazaji wa utalii ndani na nje ya nchi ni masuala muhimu katika kuvutia watalii wengi zaidi kuja hapa nchini.
Kwa kuzingatia hilo, Serikali hivi sasa iko katika hatua za awali za kuiunda upya Bodi ya Utalii Tanzania ili kuifanya Mamlaka ya Utalii Tanzania ambapo pamoja na jukumu lake kuu la utangazaji utalii, itawajibika pia kudhibiti huduma na kusimamia shughuli zinazohusiana na utalii, ikiwa ni pamoja na kusajili kampuni za kitalii.
Hatua hii inalenga kukiboresha chombo hiki, kukiimarisha na kukipa nguvu zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Ndugu Mwenyekiti,
Ninafahamu kuwa hivi sasa Bodi ya Utalii Tanzania kwa kushirikiana na sekta binafsi ipo katika mchakato wa kutayarisha mkakati mpya wa utangazaji utalii wa taifa. Napenda kuwatia shime katika hili na ninaamini kabisa utekelezaji wa mkakati huu utasaidia sana katika kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu.
Serikali inatambua changamoto zinazoikabili Bodi ya Utalii na hasa ufinyu wa bajeti katika kutekeleza majukumu yake. Kwa sasa Bodi inategemea kwa asilimia mia moja ruzuku kutoka serikali kuu ambayo haitoshelezi mahitaji ya Bodi. Kwa kiasi kikubwa ufinyu huu wa bajeti unatokana na serikali kuelemewa na majukumu mengine katika sekta nyingine kama vile afya, elimu, usafiri, kilimo, na kadhalika. Ni matumaini yangu kuwa changamoto hii itapungua kwa kiasi kikubwa pale utaratibu wa tozo ya kitanda siku utakapoanza.
Ndugu Mwenyekiti na
Ndugu Wakurugenzi,
Mafanikio ya Bodi ya Utalii Tanzania na mengineyo mengi ambayo sikuyataja yametokana na ushirikiano mzuri baina ya Wakurugenzi wa Bodi zilizopita, Menejimenti ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na wafanyakazi wote kwa jumla. Kwa mantiki hiyo, ndugu Mwenyekiti na Bodi yako, ninyi ndio wadau wakuu na chachu ya mafanikio na maendeleo ya Bodi hii. Hivyo naomba nitumie fursa hii kuwakumbusha baadhi ya wajibu na majukumu mliyonayo kwa chombo hiki:
(i) Kuidhinisha mikakati na mipango ya muda mfupi na mrefu ya kutangaza utalii na kuona inatekelezwa ipasavyo;
(ii) Kuidhinisha bajeti za Bodi ya Utalii na kushauri Wizara/Serikali kuhusu mbinu za kuboresha bajeti ya utangazaji utalii;
(iii) Kuishauri serikali juu ya mipango ya kukuza utalii na kuona jinsi Bodi ya Utalii inavyoweza kutoa mchango wake;
(iv) Kuishauri serikali katika masula yanayohusu sera ya utalii, sheria na kanuni zinazohusu ukuzaji na utangazaji utalii;
(v) Kuiongoza Menejimenti katika kukuza maslahi bora ya wafanyakazi waBodi ili kuongeza ari ya kufanya kazi kwa ustadi na ufanisi; na
(vi) Kuwa mlinzi msimamizi (watchdog) katika masuala mbalimbali yanayohusu kukuza utalii na kwa hiyo kukuza pato kutokana na utalii.
Ndugu Mwenyekiti,
Pamoja na majukumu hayo niliyoyataja, ningependa kuwapa majukumu mahsusi katika miaka hii mitatu ya utumishi wenu,msimamie maeneo yafuatayo:
(i) Ningependa kuona kwamba wigo wa utalii unapanuka, zaidi ya utalii wa wanyamapori (wildlife tourism);
(ii) Katika mkakati mpya wa utangazaji utalii, Ni vema suala la 'branding nchi' yetu lisimamiwe na kukamilisha mwaka huu.

(iii) Kuwepo mbinu mpya na za kisasa za utangazaji utalii hii ikiwa ni pamoja na ukamilishaji na utekelezaji wa mkakati wa utangazaji na ukuzaji utalii wa miaka 5 ijayo (TOURISM MASTER PLAN 2012-16) ikihusisha matumizi ya njia za kielektroniki kutangaza (e-Marketing);Lengo liwe ni kufikia watalii million 1 mwishoni mwa 2013 na kuhakikisha utalii unaendelea kukua kwa asilimia 8-10 kwa mwaka na hivyo kufikia walau watalii milioni 1.2 ifikapo 2015.

(iv) Kuboresha mkakati wa uendelezaji na utangazaji utalii wa ndani (Domestic Tourism Marketing Strategy);

(v) Kuiongoza Bodi ya Utalii iwe na vyanzo binafsi vya fedha kupitia vitega uchumi mbalimbali;

(vi) Kuikuza Bodi kama kitaasisi ili kuwa na uwakilishi (mawakala) kwenye Nchi ambazo ni vyanzo muhimu vya watalii. Aidha, ni vema Bodi kusaidia kuanzishwa Bodi ndogondogo za Utalii za Kimikoa na kuwa na maofisa wawakilishi (liason officers) kwenye maeneo hayo ya mikoa. Na,

(vii) Kusimamia vizuri ‘migration’ ya Bodi ya Utalii kutoka ilivyo sasa kama Bodi ya Utangazaji Utalii kwenda kuwa Mamlaka kwa kushirikiana na Idara ya Utalii.

Ndugu Mwenyekiti,
Majukumu haya mnayokabidhiwa leo ni makubwa. Ni matarajio yangu binafsi na serikali kwamba kwa kutumia uzoefu na maarifa mliyonayo na kwa kushirikiana na Menejimenti ya Bodi ya Utalii, mtaweza kukiongoza vema chombo hiki, na mtakuwa kiungo madhubuti baina ya Wizara, Bodi ya utalii, sekta binafsi na sekta ya umma kwa ujumla.
Aidha, naelewa uzoefu, umahiri na weledi mlionao wewe Mwenyekiti na wakurugenzi wengine, ninawafahamu, sijabahatisha kuwateua, hivyo, mkidhamiria hamtaniangusha mimi wala taifa na sina shaka kabisa mtakuwa msaada mkubwa sana kwa Bodi ya Utalii Tanzania. Nyote kwa ujumla mtatumia ujuzi na uzoefu wenu katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Bodi ya Utalii.
Ni matarajio yangu makubwa pia kuwa chini ya uongozi wako ndugu Mwenyekiti, Bodi itaendelea kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Bodi ya Utalii na wadau wengine katika sekta ya utalii nchini yataendelea kuimarishwa zaidi kwa manufaa ya sekta hii na Taifa kwa ujumla.
Napenda nikuhakikishie ndugu Mwenyekiti kwamba Wizara yangu itaendelea kutoa ushirikiano kwa Bodi yako ili iweze kutekeleza majukumu haya niliyoyataja hapo juu kikamilifu.
Ndugu Mwenyekiti,
Naomba sasa nitumie nafasi hii kabla sijahitimisha hotuba yangu kuishukuru Menejimenti na wafanyakazi wote wa Bodi ya Utalii Tanzania kwa ushirikiano walioipa Bodi ya Wakurugenzi iliyopita. Ushirikiano wao uliwezesha kufanikisha kwa kiasi kikubwa malengo ambayo walipewa katika kutekeleza majukumu ya kutangaza utalii. Ni matumaini yangu kwamba Menejimenti na wafanyakazi wote wataendelea kutoa ushirikiano huo kwako wewe Mwenyekiti na Wakurugenzi wa Bodi ili majukumu yaliyo mbele yenu yaendelee kutekelezwa ipasavyo.
Ndugu Mwenyekiti na Wakurugenzi wa Bodi, baada ya kusema hayo ninayo furaha kutamka rasmi kuwa, Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania sasa imezinduliwa rasmi.
Mhe Ezekiel Maige (MB)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
5 Aprili 2012

No comments: