Friday, April 6, 2012

Mtazamo Wangu: Tume Ya Katiba Iwe Ya Kurudisha Imani Kwa Watanzania




Ndugu zangu,

Mchana wa leo zimetufikia habari. Rais Jakaya Kikwete ameteua Tume ya Katiba yenye wajumbe 30. Tume inaongozwa na Majaji Wastaafu; Jaji Joseph Warioba kama Mwenyekiti na Jaji Augustino Ramadhan kama Makamu wake.

Hii ni hatua ya kupongezwa kwa wote waliofanikisha kutufikisha hapa wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete. Hata hivyo, kwenye safari hii ya kuelekea kwenye kuandika Katiba Mpya,  kuna changamoto  nyingi na baadhi ni ngumu.

Na hakika, tulipofikia  sasa, kikubwa kinachokosekana miongoni mwetu Watanzania ni IMANI.  Mchakato mzima wa kudai Katiba Mpya, tangu ulivyoanza miaka ya 1990, ulitawaliwa na hali ya kutoaminiana. Hali ya kukosekana kwa imani ingalipo.

Hivyo basi, changamoto ya kwanza kabisa kwa Tume iliyoundwa ni kufanya kazi ya kuandaa rasimu ya Katiba itakayowarudishia imani Watanzania juu ya dhamira ya Serikali ya kutaka kuwepo kwa Katiba itakayoifanya Tanzania iwe nchi ya kisasa. Kwamba Katiba ichangie kwenye  kuwarudishia imani Watanzania juu ya namna watakavyoendesha nchi yao.

Hakika, tatizo letu kubwa kwa sasa ni kukosekana kwa imani miongoni mwetu . Hatuaminiani. Ndio maana, Serikali nyingi Afrika hazipendi kuwepo kwa Tume Huru za Uchaguzi kwa vile hutoa nafasi kwa walio kwenye upinzani kuingia madarakani. Na kwa vile hawana imani nao mara nao watakapoingia madarakani, basi, Serikali hizo huona ni vema kutokuwepo kwa Tume Huru za Uchaguzi.

Kama Tume hii iliyoundwa hii leo itapendekeza kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi , basi, huo utakuwa ni mwanzo wa mapinduzi makubwa ya kuifanya nchi yetu kuwa ya kisasa zaidi.  Nahofia, Tume Huru ya Uchaguzi itasubiri mpaka tuchinjane kwanza kwa kutuhumiana kuibiana kura kwenye chaguzi. Tatizo ambalo lingeweza kumalizwa kwa kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi itakayoaminika na pande zote zinazoshiriki chaguzi.

Tukumbuke, kuwa  imani ikikosekana hususan kwa vyama na wananchi dhidi ya Serikali katika kuandika Katiba hii, basi,  kutaufanya  mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya uwe ni wa gharama kubwa bila matunda tarajiwa kwa umma.

Kuna wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki- Moon alitamka; kuwa tatizo kubwa la Serikali nyingi si nakisi ya bajeti bali nakisi ya imani ya Wananchi kwa Serikali hizo. Ndio, kupungua kwa imani. Ndio, inahusu imani na ni wajibu wa Serikali na Chama cha Mapinduzi kuirudisha imani ya wananchi kwa Serikali na chama hicho.


Nimepata kuandika, kuwa nchi yetu iko njia panda. Mbele yetu kuna njia mbili; moja inaelekea tunakopita sasa. Kwenye hali ya ’ kujifunga’ na kubaki tulipo bila kupiga hatua za haraka za maendeleo huku baadhi, wakiwamo viongozi, wakiwa na udhibiti mkubwa wa hali ya mambo. Njia nyingine inaelekea kwenye uhuru zaidi wa wananchi na uwezo wa kuwadhibiti na kuwawajibisha viongozi wao. Ni njia inayoelekea kwenye ustawi wa nchi. 

Watanzania wengi kwa sasa wana kiu kubwa ya kuianza safari ya kuipita njia ya pili. Njia yenye uhuru zaidi na matumaini ya ustawi wa taifa. Njia itakayotufanya tuondokane kabisa na njia ya kwanza, njia inayotufunga na kutubakisha hapa tulipo. 
Tume iliyoundwa leo na Mheshimiwa Rais Kikwete itusaidie  kutupitisha kwenye njia ya pili; Njia yenye uhuru zaidi na matumaini ya ustawi wa taifa.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Maggid Mjengwa, 
0788 111 765

No comments: