Wednesday, April 18, 2012

KAMATI YA NIDHAMU YATUPA RUFANI YA YANGA



Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Aprili 17 mwaka huu) imetupa rufani ya Yanga iliyowasilishwa mbele yake kupinga uamuzi wa kupokwa pointi tatu kwa kumchezesha mchezaji asiyestahili.

Aprili 2 mwaka huu Kamati ya Ligi ya TFF iliipa Coastal Union ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Yanga kumchezesha beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu hizo iliyofanyika Machi 31 mwaka huu wakati akiwa na adhabu ya kukosa mechi tatu.

Yanga katika rufani hiyo iliwasilisha sababu nane za kupinga kupokwa pointi hizo, kubwa zikiwa Cannavaro hakustahili kutumikia adhabu ya kukosa mechi tatu, si aliyempiga refa Israel Nkongo, ripoti za refa na kamishna wa mechi yao dhidi ya Azam zilionesha dalili ya njama (conspiracy) kwani zilifanana.

Pia Cannavaro alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao adhabu zao zilisimamishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, Kamishna mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana.

Katika uamuzi wake, Kamati imesema adhabu ya Cannavaro ya kukosa mechi tatu kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ya Ligi Kuu ya Vodacom ilitolewa na refa na si Kamati ya Ligi kama ambavyo inalalamikiwa na Yanga, na kanuni hiyo haikatiwi rufani.

Pia barua ambayo TFF iliiandikia Yanga kuhusu adhabu ya mchezaji huyo ilikuwa wazi kwani ilikariri kanuni ya 25(c), hivyo kitendo cha klabu hiyo kumtumia mchezaji huyo ulikuwa ni uzembe wa kutoheshimu kanuni. Kama Yanga haikufahamu vizuri kanuni hiyo ilikuwa na fursa ya kuiandikia TFF kwa mujibu wa Kanuni ya 25(f) ili kupata ufafanuzi kabla ya kuamua kumtumia mchezaji huyo.

Vilevile adhabu zilizokuwa zimesimamishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ni zile ambazo zilikuwa zimetolewa na Kamati ya Ligi, na si zile zilizotolewa uwanjani na refa.

Kuhusu madai ya conspiracy kwa ripoti za kamishna wa mchezo huo na refa, Kamati imebaini kuwa hazifanani, na suala lililokuwa likibishaniwa (contentious issue) lilikuwa ni kunyang’anywa pointi tatu.

Pia Kamati ilikariri Ibara ya 50 ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuwa mchezaji anayembughudhi refa kwa njia yoyote ile anastahili kufungiwa kwa angalau mechi sita.

No comments: