Wednesday, April 18, 2012

Neno Fupi La Jioni Hii: Mshindi Mzuri Ni Yupi?


Ndugu zangu, 

Siku ya leo imekuwa na ushindani mwingi. Tangu saa tatu asubuhi kumekuwa na hali ya wagombea Ubunge Afrika Mashariki kujieleza na kuulizwa maswali.

Na usiku huu Bayern Munchen wanapambana na Real Madrid. Ni kuwania taji la Ubingwa wa Kombe la Washindi. Ni ushindani mwingine. Ndio, hata washindi hushindanishwa, na ni mmoja tu ndiye atakayekuwa mshindi wa washindi wote. Hivyo, walio nyuma yake watakuwa wameshindwa.

Naam, panapo ushindani kuna kushinda na kushindwa. Busara kwa mwanadamu ni kujitayarisha na kushinda au kushindwa. Na siku zote kuna mshindi mzuri na mbaya, vile vile kuna mshindwa mzuri na mbaya. Wenye hulka hizo hujionyesha kwa kauli na matendo yao. 

William Malecela ni mfano wa mshindwa mzuri. Nilifuatilia maelezo yake pale Bungeni. Kama wenzake, naye alipambana, lakini ameshindwa. Na haraka amekiri kushindwa bila kulalamika. Amewapongeza washindi na amewafariji washindwa wenzake. Huo ndio ukomavu wa kisiasa. Namtakia kaka William kila la kheir. Naamini atarudi tena na hata kushinda, maana, sasa amepata uzoefu mpya. Ni zoefu wa kushindwa. Kuna wengi wasio na uzoefu wa kushindwa. Shyrose Banji ni mfano wa wenye uzoefu mkubwa wa kushindwa. Nampa hongera nyingi kwa hatimaye kushinda!

Na Mzee Ali Hassan Mwinyi ni mfano wa mshindi mzuri. Nakumbuka nilikuwa nje ya ukumbi wa Diamond mwaka 1985. Ni pale Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi alipotoa hotuba ya kushukuru kuteuliwa kugombea Urais na kumrithi Mwalimu Nyerere. Nakumbuka kauli yake hii; 

“ Nduguzanguni, kama mtanilinganisha miye na Mwalimu Nyerere,basi, ni sawa na kulinganisha Mlima Kilimanjaro na kichuguu”. Hiyo ni kauli kutoka kwa mtu mwuungwana, mnyenyekevu na asiye na majivuno.

Babu zetu walipokwenda vitani, moja ya mambo yaliyokuwa ni mwiko kumfanyia adui ni kitendo cha kumchoma mkuki au kumkanyaga adui alieanguka chini huku akiwa hajiwezi . Maana, mshindi mzuri hana majivuno. Hatoi kauli za kumdhalilisha mpinzani wake. Mshindi mzuri ni mnyenyekevu. Anayajua machungu ya kushindwa, kwa vile , mshindi mzuri naye ameshindwa mara nyingi. Je, mshindwa mzuri na mbaya ni yupi? Subiri nenofupi la jioni ya kesho. Panapo Uzima. 

Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
0788 111 765


No comments: