Friday, April 13, 2012

Lissu aiomba Mahakama itupe kesi dhidi yake

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki,
Tundu Lissu


Mlalamikiwa wa kwanza, kesi ya kupinga matokeo ya ubunge, Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, ameiomba mahakama kutupilia mbali shauri hilo na iamuru walalamikaji kulipa gaharama , kutokana na ushahidi wa ovyo uliotolewa mahakamani.
Alisema hayo wakati akijitetea, kufuatia upande wa walalamikaji kufunga  baada ya mashahidi 24 kutoa ushahidi mbele ya Jaji Moses Mzuna wa Mahakama Kuu Kanda ya Kilimanjaro.
Lissu aliieleza Mahakama kuwa mashahidi waliotoa ushahidi hakuna hata mmoja aliyemtaja wazi kuwa alinunua au aliruhusu juisi, biskuti na maji, wapewe mawakala waliokuwa wanasimamia kura zake.
“Mawakala wa Chadema walijitoa kufanya kazi hadi saa 12 jioni, wengine hadi saa tano usiku kuhakikisha kura haziibiwi, walijitolea hawakupewa hata senti moja…maneno ya watu wengine ya kushinikiza tu, walioshindwa kwenye uchaguzi, wanatafuta vijisababu vyao,” alisema.

Aidha, Lissu alikiri kufanya sherehe Machi 12, 2011 huko Mungaa, Singida Vijijini ili kupongeza wananchi na mawakala waliosimamia kura na kuvitaja vyama vya APPT-Maendeleo, NCCR-Mageuzi na Chadema, kuwa vilisimamia kura zao vizuri.
Hata hivyo, Lissu aliieleza Mahakama kuwa, shahidi wa 21, William Swai, Afisa Tarafa Mungaa walikuwa na ugomvi wa siku nyingi, kabla hata ya uchaguzi na alilumbana naye katika mikutano yake tangu 2008 hadi 2010, akidai kibali cha mkutano, kila alipotaka kuhutubia wananchi.
Alidai kuwa hakushangaa kumuona Swai akitoa ushahidi wa uongo mahakamani kuwa, siku ya mkutano wa kushukuru wananchi waliomchagua, yeye (Lissu). Pia Lissu aliieleza Mahakama kuwa kushangazwa na madai ya walalamiakaji kuwa, Jonathan Njau, waliyogombea naye, alikataa kusaini matokeo, wakati hakuwepo kwenye ukumbi wa majumuisho, badala yake aliwakilishwa na mtu mwingine.
Alidai kuwa wakati yeye alilala kituo cha kujumuisha kura kwa siku mbili kukusubiri matokeo, mwenzake hakuwepo, badala yake aliwakilishwa na mlalamikaji wa kwanza, Shaban Itambu Selema. Lissu aliongeza kuwa iwapo muda wa kutosha ungekuwepo kwa ajili ya kesi hiyo,  Njau angeitwa kutoa ushahidi wake, kutokana na jinsi alivyotajwa na kuguswa mara nyingi katika kesi hiyo.
“Mheshimiwa Jaji, nguvu ya fedha ni suala muhimu sana katika kesi hii, kuna nguvu kubwa sana zipo gizani zimejificha, zinachochea kesi hii, zinatoa fedha, kutafuta kichwa cha Lissu kwenye sahani, kama vile kichwa cha Yohana mbatizaji kilivyotafutwa,”  alidai.
CHANZO: NIPASHE

No comments: