Friday, April 13, 2012

Baraza la Habari Tanzania:Acheni Mahakama ifanye Kazi Yake Juu Ya Kifo Cha Steven Kanumba



Kutoka
kulia ni Katibu wa MCT Kajubi Mukajanga katikati ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Maadili Baraza la Habari MCT  Jaji Thomas B. Mihayo na
 Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili pia Mjumbe wa Bodi Rose Haji.
Picha: Blasio Kachuchu

---

KAMATI ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) leo  mchana
imetangaza  imesikitishwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili uliojitokeza
hivi karibuni kwa baadhi ya vyombo vya Habari ambavyo wakati vikiripoti
kuhusu kifo cha Msanii Steven Charles Kanumba, vimemhukumu msichana
Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu, kuwa amemuua msanii huyo.


Ukiukwaji
huo umejitokeza hasa baada ya msichana huyo kufikishwa Mahakamani,
ambapo baadhi ya magazeti yanayoheshimika katika jamii jana Alhamisi,
Aprili 12, 2012 yaliandika vichwa vikubwa vilivyosomeka: Lulu Kortini
kwa kumuua Kanumba na Lulu Kizimbani kwa mauaji ya Kanumba.


Kwa
mujibu wa sheria na maadili ya Uandishi wa Habari mtu yeyote
anayekamatwa kwa tuhuma yoyote ile ni mtuhumiwa mpaka atiwe hatiani na
mahakama.


Kanuni hii ya siku nyingi katika fani ya uandishi wa habari inafahamika na waandishi na wahariri wote wanaoheshimu kazi yao.


Baraza
pia limeshatoa matamko mara kadhaa kuwakumbusha wanahabari kujiepusha
na uandishi wa habari au vichwa vya habari vinavyohukumu.


Baraza
linafahamu fika kuwa kesi zilizoko Mahakamani ni kivutio kwa umaa
kutaka kujua kinachoendelea ili kuona haki ikitendeka na pia wanahabari
wana haki ya kujua na kuripoti yanayojiri huko na katika vyombo vingine
vya sheria.


Lakini
lazima ifahamike kuwa wakati wakitumia fursa na haki hiyo Wanahabari
wanapaswa kuzingatia kanuni, miongozo na sheria zinazolinda haki za
msingi zxa watuhumiwa na uhuru wa Mahakama.


Ni
wazi kuwa vichwa vya habari vilivyoitajwa hapo juu vimeliingilia uhuru
wa Mahakama kwa kuchapisha habari ambazo zinaonekana kushawishi au
kushinikiza uamuzi wa Mahakama.


Wanahabari
ni lazima watambue kuwa kuna taratibu na makubaliano ya kijamii juu ya
namna gani taarifa zinavyopaswa kuripotiwa ili kutowadhuru watu wengine.


Hivyo
basi , Baraza la Habari Tanzania linapenda kuwakumbusha tena wahariri
kuhakikisha kuwa wanafanya kazi yao kwa kuzingatia maadili na weledi
katika kuripoti mkasa huu unaogusa hisia za watu.


Imesainiwa na
Jaji Thomas B. Mihayo
Mwenyekiti,Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania.

No comments: