Tuesday, April 17, 2012

Maggid Mjengwa na Neno La Leo: Siasa Hizi Za Ki-Hodorono!

Ndugu zangu,


Sisi wa Kizazi Cha Azimio na wanyuma yetu bado tuna kumbukumbu ya ' Senema za Omo'.


Mara moja kwa mwezi ' tabaka la Wafanyakazi' wengi wakiishi Ilala
lilikuwa likionyeshwa filamu. Hawa ni wazazi wetu wakati huo. Ilala ni
karibu na eneo la viwandani kule Pugu Road.


Pale viwanja vya Shule ya Msingi ilikuwa ni moja ya sehemu za wananchi kukusanyika kuangalia senema ya bure.


Hakukuwa na televisheni enzi hizo na filamu ya picha zinazotembea kwenye
kitaambaa kikubwa cheupe ilikuwa jambo la kuvutia sana. Na kwenye '
Senema za Omo' ndipo tulipokuwa tukionyeshwa matangazo ya biashara pia.


Nilikuwa mdogo sana, lakini, moja ya matangazo ninayoyakumbuka sana ni
tangazo la Hodorono. Haya ni manukato ya kujipulizia makwapani ama
maarufu kwa jina la perfume.


Tulionyeshwa abiria anayeingia kwenye basi, na mara abiria mmoja huku
akiwa ameshika pua akaanza kutamka kwa sauti; " Hodorono! Hodorono!". Na
wengine wakaitikia " Hodorono! Hodorono! Hodorono! Huku wakitokea
madirishani. Mwisho kwenye basi akabaki abiria yule aliyeingia.
Akaonekana aliyeshangaa asijue kilichowafukuza wenzake. Ujumbe ukawa
umefika kwake na jamii, kuwa tutumie Hodorono!
Miaka mingi imepita tangu nilione tangazo lile. Katika fikra zangu hizi
za ukubwani, tangazo lile si kingine bali ni tangazo la kibaguzi na
ambalo halikufaa kuonyeshwa katika jamii.


Na siasa zetu za siku hizi nazo zimekuwa za staili ya Hodorono. Ni siasa za kibaguzi unausukumwa na ubinafsi.


Tunaona vijana wa leo wameanza kuukataa kwa vitendo ubaguzi huu wa
kisiasa. Ni jambo jema. Huko nyuma TANU na baadae CCM viliamini kuwa
asiyefikiri kama wao basi si mwenzao. Ni mpinzani, ni adui wa maendeleo.
Ni adui wa umma. Ni msaliti. Si mwenzao na alibaguliwa. Alitengwa na
pengine kuishia kifungo cha ndani au cha nje kwa kurudishwa kijijini
alikozaliwa au asikozaliwa.


Huko Mtanzania huyo aliyebaguliwa kisiasa alifikia kuambiwa kuwa kila
siku awe anaripoti kwa Balozi wa Nyumba Kumi. Na kutoka kijijini kwake
kwenda kijiji kingine ni sharti aombe ruhusa ya uongozi wa kijiji! Na
kutoka nje ya wilaya ni sharti apate kibali cha DC! Hii nayo ni historia
yetu. Ili tuelewe tulipo na tunakokwenda tuna lazima ya kuipitia
historia yetu.

Ubaguzi wa kisiasa ni jambo baya sana. Kwamba kuna wanaojiona wao wana
haki zaidi kuliko wenzao katika nchi hiyo hiyo ambayo wenzao pia
wanaiiita nchi waliyozaliwa. Kwamba wana uwezo wa kuwafanya Watanzania
wenzao waishi maisha magumu kwa vile tu wanatofautiana au wanapingana
kifikra na walio kwenye mamlaka ya dola au Chama kilicho madarakani.

Ubaguzi wa kisiasa huzaa chuki ya kisiasa. Na mara zote, uvumilivu wa
wanaobaguliwa na kukandamizwa hufikia kikomo. Na yanapolipuka, basi,
huwa kama nusu ya kiyama. Moto huwaka. Hakukaliki.

Kule Misri vijana wengi wanajua sasa ni kwanini wazazi wao walihangaika
sana kutafuta ajira lakini hawakupata na kuishia kuishi maisha magumu.
Wanajua sasa ni kwanini baadhi yao ( Vijana) hawakupata scholarship au
ajira baada ya kufuzu masomo yao.

Wanajua sasa, kuwa Idara ya Usalama wa Taifa chini ya Hosni Mubarak,
familia yake na jamaa zake wa karibu walikuwa na faili maalumu yenye
orodha ya majina ya WaMisri, vijana kwa watu wazima, ambao walionekana
kuwa ni wenye fikra za kipinzani. Kuna waliochunguzwa tangu wakiwa
kwenye mijadala ya vyuo vikuu. Na ambaye jina lake limeingizwa kwenye
faili hilo, basi, ataandika kurasa kwa maelfu za barua za maombi ya
kazi, na atasaga lami sana hadi soli za viatu ziishe akitafuta ajira
bila mafanikio. Serikali ya Hosni Mubarak ilikuwa na mikono mirefu, na
miguu pia. Tatizo lilikuwa kwenye 'kichwa cha Serikali'. Kilikuwa kidogo
sana, maana hatma ya yaliyomfika Hosni Mubarak ingepaswa kuepukwa na
mtu mwenye kichwa kinachofikiri. Kwa vile kilichotokea kingetokea,
ilikuwa ni suala la wakati tu.

Ndio, Usalama wa Taifa ( Zaidi Usalama wa Hosni Mubarak na Chama chake)
ulihakikisha Mmisri ambaye jina lake limo kwenye kitabu chao hapati kazi
yeyote ile labda iwe ya kubeba zege ili hali ana digrii ya chuo Kikuu.

Nimefurahi sana hii leo kuwasilimulia juu ya tangazo la Hodorono kwenye enzi za utoto wangu. Hakika, ni tangazo la kibaguzi.

Na siasa zetu siku hizi zimekuwa za Ki-Hodorono. Ni siasa za kibaguzi.
Tunajenga nyumba moja, lakini tunagombania fito. Ni hulka za ubinafsi.
Kama nchi , siasa za hodorono zitatupelekea si tu kuvuja jasho na
makwapa kunuka, bali kuvuja damu kwa kukatana mapanga. Kwa viongozi
tuliowapa dhamana kutotanguliza busara na hekima.


Na hilo ni Neno La Leo.

Maggid Mjengwa,

Dar es Salaam.

0788 111 765

No comments: