Wednesday, April 11, 2012

Msama ashukuru waliofanikisha tamasha la Pasaka




MWENYEKITI wa iliyokuwa Kamati ya Maandalizi ya tamasha la Pasaka, Alex Msama amewashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha tamasha hilo kwa hali na mali.



Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Dodoma jana, Msama ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions aliyeandaa tamasha hilo lililofanyika Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Jumatatu ya Pasaka kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, alisema anaamini Mungu atawajazia zaidi wote waliotoa michango kufanikisha tamasha hilo.

Tamasha hilo lilikuwa na lengo la kuchangia sh. milioni 50 kwa wasiojiweza wakiwamo watoto yatima na wanawake wajane.

Katika tamasha hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, pamoja na marafiki zake alioongozana nao jukwaani walichangia sh. milioni 10, akasema Rais Kikwete pia aliahidi kuchangia sh. milioni 10 na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda sh. milioni 5, hivyo kufanya jumla kuwa sh. milioni 25, zitakakazotumika kusaidia wasiojiweza.

Pia katika tamasha la Dodoma juzi, Naibu Spika, Job Ndugai alichangia sh. milioni 2 kwenye mfuko huo.

"Siwezi kumtaja kila mmoja kwa jina, lakini napenda kumshukuru kila mmoja aliyefanikisha tamasha hilo ikiwa ni pamoja na mashabiki waliomiminika kwa wingi kushuhudia Dar es Salaam na Dodoma," alisema Msama.

Msama pia alikanusha taarifa iliyoripotiwa kwenye gazeti moja la kila siku (si Jambo Leo) kuwa Membe alizomewa huku akioneshwa alama ya vidole viwili inayotumiwa na Chadema, na umati wa waumini waliojaa pomoni Uwanja wa Taifa, alipokuwa akihutubia.

Tamasha hilo lilipambwa na wasanii kochokocho waliokonga nyoyo za mashabiki wakiwemo, Rebecca Malope kutoka Aftrika Kusini, Solomon Mukubwa, Anastazia Mukabwa, Maryanne Tutuma kutoka Kenya, Ephraim Sekeleti wa Zambia, Rose Muhando, Upendo Kilahiro, Christina Shusho, John Lissu, kundi la Glorious Celebration na kwaya ya Kinondoni Revival.


No comments: