Wednesday, April 11, 2012

RAIS KIKWETE AOMBOLEZA KIFO CHA MKUU WA MAJESHI MSTAAFU JENERALI ERNEST MWITA KYARO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Mstaafu Ernest Mwita Kyaro.
Jenerali Mstaafu Ernest Mwita Kyaro ameaga dunia saa nne asubuhi leo, Jumanne, Aprili 10, 2012 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza,  akiwa na umri wa miaka 87.
Katika salamu zake kwa Jenerali Mwamunyange, Rais Kikwete amemwomba Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi kumfikishia salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa familia ya Jenerali Mstaafu Kyaro na kwa makamanda na wapiganaji wote wa Majeshi ya Ulinzi kwa kumpoteza mdau, mwenzi wao na kiongozi wao.
Rais Kikwete amesema katika salamu zake, “Nimepokea kwa huzuni nyingi na majonzi mkubwa taarifa ya kifo cha Jenerali Mstaafu Ernest Mwita Kyaro ambaye ameaga dunia asubuhi ya leo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza, ambako alikuwa amelazwa.”
“Nilifahamu vizuri na nilifanya kazi na Jenerali Kyaro wakati wa enzi ya uhai wake.  Alikuwa Mtanzania mzalendo wa kuigwa, mwadilifu na mwaminifu kwa taifa lake, mchapakazi hodari na mpiganaji na kamanda wa mfano kabisa kwa waliokuwa chini yake, “  amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Alithibitisha sifa zake hizo katika kipindi chote cha miaka 50 na miezi 11 alipokuwa katika ulinzi wa nchi yetu, tokea alipokuwa mpiganaji hadi alipopanda na kuwa kamanda na hatimaye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kwa kipindi cha miaka minne kati ya 1988 hadi Februari 25, 1992, alipostaafu utumishi wa Jeshi. Tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi kwa utumishi wake uliotukuka kwa taifa letu.”
Rais Kikwete ameongeza: “Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange salamu zangu za rambirambi kufuatia kifo cha Jenerali Kyaro.  Naomba pia kupitia kwako uniwasilishie salamu nyingi za rambirambi za dhati ya moyo wangu kwa wanafamilia wa Mzee Kyaro ambao wameondokewa na baba, babu na mhimili mkuu wa familia yao.”
“Aidha, kupitia kwako uniwasilishie salamu zangu kwa makamanda na wapiganaji wote wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ambayo yamempoteza mdau, mwenzi wao na kiongozi wako.  Wajulishe wanafamilia, makamanda na wapiganaji wote kuwa niko nao kwa sababu huu ni msiba wetu sote.  Nawaombea moyo wa subira katika kipindi hiki na naungana nao wote katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweka pema peponi roho ya Marehemu Ernest Mwita Kyaro. Amen.”
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
10 Aprili, 2012

No comments: