Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta-Jenerali Saidi Mwema kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta-Jenerali Mstaafu Harun Mahundi (pichani).
Marehemu Harun Guido Mahundi ambaye alikuwa Inspekta-Jenerali wa Polisi kwa miaka 10 kuanzia mwaka 1985 amefariki dunia leo, Jumatatu, Aprili 2, 2012, mjini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 72.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Inspekta- Jenerali Mwema, Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kuhuzunishwa na habari za kifo cha Marehemu Mahundi ambaye katika enzi za uhai wake alikuwa mtumishi mwaminifu, mwadilifu na wa kutumiwa wa umma.
“Nimeshtushwa na huzunishwa na habari za kifo cha Marehemu Mahundi ambaye katika enzi zake nilimfahamu kama mtumishi mwaminifu, mwadilifu na wa kutumainiwa wa umma,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tokea alipojiunga na Jeshi la Polisi kama Konstebo mwaka 1960 hadi utumishi wake kama Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha na hadi kuteuliwa kwake kuwa Inspekta-Jenerali wa Polisi, Harun Mahundi alithibitisha kuwa mtu wa kuaminiwa katika jamii na katika utumishi wa umma.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Alikuwa pia mfano mzuri wa kujiendeleza katika maisha kama alivyofanya wakati aliposomea na kupata shahada ya sheria mwaka 1978 akiwa ndani ya utumishi wa umma. Hata baada ya kustaafu Jeshi la Polisi aliendelea kuwa mfano wa kuigwa katika jamii katika nafasi zake nyingine kama Kamishna wa Tume ya Uchaguzi na mwanasheria wa kujitegemea.”
Rais amemwambia Inspekta-Jenerali Mwema: “Nakutumia wewe binafsi na kupitia kwako kwa Makamanda na askari wa Jeshi zima la Polisi salamu zangu za rambirambi kufuatia kifo cha Mzee Mahundi.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Aidha, kupitia kwako, naomba uniwasilishie salamu za dhati ya moyo wangu kwa familia yote ya Marehemu Mahundi. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa na kuwa nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Wajulishe pia kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ailaze pema peponi roho ya Marehamu. Amen.”
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
02 Aprili, 2012
No comments:
Post a Comment