Monday, April 2, 2012

Rose Muhando" Utamu wa Yesu mtauona Pasaka"


MWIMBAJI nguli wa muziki wa Injili nchini, Rose Muhando ameahidi kukonga nyoyo za mashabiki wa muziki huo watakaojitokeza kushuhudia tamasha la Pasaka litakalorindima Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 8 mwaka huu.



Rose amesema atatumia fursa hiyo kutambulisha nyimbo zake saba zilizomo katika albamu yake ya Utamu wa Yesu ambazo ni Utamu wa Yesu uliobeba jina la albamu hiyo, Raha Tupu, Tamalaki, Ndivyo Ulivyo, Woga Wako, Imbeni na Kusifu na Achia.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Rose alisema pia katika tamasha hilo atapata wasaa wa kuimba kwa kushirikiana na mwanamuziki wa Kenya, Anastazia Mukabwa, aliyeimba kwa kumshirikisha kwenye katika wimbo wa Vua Kiatu.

Tamasha hilo litasindikizwa na wasanii kochokocho wa muziki wa injili wakiwamo Rebecca Malope wa Afrika Kusini, Solomon Mukubwa, Mukabwa, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho, Atosha Kissava, Mwinjilisti Faraja Ntaboba, Ephraim Sekeleti, Maryanne Tutuma, kundi la Glorious Celebration na kwaya ya Kinondoni Revival.

Rose alisema amepania kufanya mambo makubwa zaidi ya alivyofanya alipozindua albamu zake zilizopita za Uwe Macho, Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi) na Jipange Sawa Sawa, na akawaomba mashabiki wamiminike kwa wingi uwanjani kuona mambo mazuri aliyowaandalia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama alisema tamasha hilo la Sikukuu ya Pasaka mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Uwanja wa Taifa na kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, mgeni rasmi atakuwa Naibu Spika, Job Ndugai, Jumatatu ya Pasaka Aprili 9 mwaka huu.

Tamasha hilo ambalo lengo lake kubwa ni kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mtaji wa biashara wajane, kiingilio kimetengwa katika kategoria tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti maalumu sh. 10,000.


No comments: