Thursday, April 12, 2012

SAFARI LAGER YATANGAZA KUSAIDIA TIMU YA TAIFA YA DARTS KUSHIRIKI MICHUANO YA DARTS NCHINI UGANDA

 Meneja wa Bia ya Safari Lager,Oscar Shelukindo akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutangaza kuisaidia timu ya taifa ya Darts kushiriki michezo ya Afrika Mashariki inayotarajia kuanza kufanyika kesho Ijumaa tarehe 13 April hadi siku ya Jumapili tarehe 15 April,Jijini Kampala nchini Uganda.Kulia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mchezo wa Vishale (Darts) Taifa,Gesase Waigama.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mchezo wa Vishale (Darts) Taifa,Gesase Waigama akitoa maelezo ya Mashindaano hayo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani).
Meneja wa Bia ya Safari Lager,Oscar Shelukindo akikabidhi hundi ya sh. mil 6 kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mchezo wa Vishale (Darts) Taifa,Gesase Waigama ikiwa ni sehemu ya msaada kwa timu hiyo ya Taifa ya Mchezo wa Vishale (Darts) inayoenda kushiriki Mashindano ya Afrika Mashariki inayotarajia kuanza kufanyika kesho Ijumaa tarehe 13 April hadi siku ya Jumapili tarehe 15 April,Jijini Kampala nchini Uganda.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager leo imetangaza rasmi kusaidia timu ya taifa ya Darts kushiriki michezo ya Darts ya Afrika Mashariki itakayofanyika nchini Uganda kuanzia kesho Ijumaa tarehe 13 April hadi Jumapili tarehe 15 April.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam leo, meneja wa bia ya Safari Lager Bw. Oscar Shelukindo amesema Safari Lager imesaidia kiasi cha fedha cha sh. Milioni 6 kwa Safari ya wachezaji 12 wa timu ya taifa kushiriki mashindano haya yanayotarajiwa kutimua vumbi jijini Kampala kuanzia saa nane mchana kesho. Mashindano haya yanayojulikana kama East Africa Darts Federation Tournament yanafanyika kila mwaka kwenye miji ya Afrika Mashariki na yanatarajiwa kufanyika hapa Tanzania mwakani, 2013.

“Safari Darts inaendeleza lengo lake la kusaidia kukuza zaidi mchezo wa Darts hapa Tanzania na tunapenda wachezaji wetu wapate pia uzoefu wa mechi za kimataifa kama hizi” Alisema Bw. Shelukindo. Safari Lager imekuwa ikidhamini mashindano mbalimbali ya mchezo wa Darts, na imegawa pia vifaa vya michezo kwa maeneo mbalimbali ya kuchezea Darts Dar Es Salaam na mikoani.

Naye mwenyekiti wa Taifa wa chama cha Darts cha Taifa (TADA) Bw. Gesase N. Waigama, ambaye pia ni raisi wa shirikisho la Darts Afrika Mashariki alisema timu ya Tanzania imejizatiti vizuri kutuwakilisha vema katika mashindano haya. Timu ya Taifa inatarajia kuwa na wachezaji 12 na inatarajiwa kuwa na wanaume kumi na mbili na wanawake 8.

Wachezaji wanatarajia kurudi mara baada ya mashindano Jumatatu tarehe 16 April 2012. Bw. Waigama alisema pia kwamba mapema mwezi wa sita chama cha Darts cha taifa kitaandaa mashindano makubwa yajulikanayo kama Tanzania International Open Darts Championship.

No comments: