Sunday, April 8, 2012

TAARIFA KWA UMMA:Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaendelea kuchambua wasifu wa wajumbe walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete Kuwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

 Mkurugenzi wa Habari na Uenezi na Mbunge wa Ubungo(CHADEMA)

------- 
  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaendelea kuchambua wasifu wa wajumbe walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa wajumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba. CHADEMA kitatoa tamko juu ya uteuzi wa tume husika baada ya uchambuzi kukamilika wa kutafakari iwapo uteuzi husika umezingatia matakwa ya umma na dhamira ya kujenga muafaka wa kitaifa wa kuwa na katiba mpya na bora.  Pamoja na kutaja majina ya wajumbe wa tume, CHADEMA kilitarajia kwamba Rais Jakaya Kikwete angeeleza pia ratiba ya kufanyika kwa marekebisho mengine muhimu ya awamu nyingine kuhusu bunge maalum la katiba na hatua ya kutunga katiba mpya na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki kabla ya mchakato kufikia katika hatua husika.  Katika muktadha huo, Kamati Maalum ya Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyoundwa tarehe 20 Novemba 2011 kwa ajili ya kukutana na Rais Jakaya Kikwete kuhusu sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011; itafanya kikao chake karibuni kupitia taarifa ya uchambuzi unaoendelea kufanywa juu ya uteuzi uliofanyika wa wajumbe wa tume na tamko litatolewa kwa umma kuhusu mchakato huu muhimu kwa maslahi ya taifa.  Itakumbukwa kwamba tarehe 27 na 28 Novemba 2011 Rais Kikwete alifanya mkutano wa siku mbili na viongozi wa CHADEMA kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba na pande mbili kukubaliana kuhusu haja ya sheria husika kufanyiwa marekebisho kwa mashauriano na wadau mbalimbali kwa lengo la kudumisha muafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa katiba mpya.  Kamati Maalum ya CHADEMA ilikutana tena na Rais tarehe 21 Januari 2012 Ikulu Dar es salaam ambapo kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe ilitaarifiwa hatua ambayo ilifikiwa na serikali katika kuanza kuiboresha sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 ili ikidhi mahitaji ya kujenga kuaminiana na muafaka wa kitaifa kwa mawasiliano na mashauriano na wadau mbalimbali.  Tarehe 22 Januari 2012 Kamati Kuu ilipokea na kujadili taarifa ya Kamati Maalum kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na kujulishwa hatua ambazo serikali ilifikia katika maandalizi ya kuifanyia marekebisho tajwa katika Mkutano wa Sita wa Bunge unaotarajia kuanza tarehe 31 Januari 2012.  Kamati Kuu iliamua kwamba Kamati Maalum iendelee kufanya mawasiliano na mashauriano na Rais Kikwete na Serikali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 inafanyiwa marekebisho ya msingi kabla ya mchakato wa kukusanya maoni kwa mujibu wa sheria husika haujaanza. Kamati Maalum ilitakiwa kuendelea kufuatilia utekelezaji wa maazimio matatu ya Kamati Kuu yaliyofikiwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kuhusu mchakato wa katiba mpya; maudhui ya maazimio hayo ni kama ifuatavyo:   Mosi; “kutoa elimu kwa wananchi na wadau wote juu ya ubovu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na juu ya haja ya kuwa na sheria itakayoweka utaratibu bora zaidi wa kuunda Tume Shirikishi ya Katiba kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti na Rasimu ya Katiba Mpya, Bunge Maalum la Katiba na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki”.  Pili; “Ushiriki wa CHADEMA katika mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba utategemea utayari wa Serikali ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya kimsingi katika sheria hiyo kwa lengo la kujenga muafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo”.  Tatu; “viongozi wote wa chama na wa kuchaguliwa katika ngazi zote kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara yenye lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na madhara yake kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya na bora kwa nchi yetu kwa lengo la kuunganisha umma wa watanzania kuweza kufanya mabadiliko ya msingi”Imetolewa 
tarehe 07 Aprili 2012 
na: John Mnyika (Mb)

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

No comments: