Friday, April 20, 2012

TAFSIRI YA MDAU MJENGWA KWA ZITTO KABWE NA SAINI 70 ZA KUMG'OA PINDA



Ndugu zangu,

Leo asubuhi wakati nikifanya ' jogging' kwenye mitaa ya Dar es Salaam niliwasikia watu wa kawaida kabisa wakijiuliza na kujadili; " inakuwaje Serikali iwalipe marehemu mishahara huku sisi tulio hai hatuna hata uhakika wa milo miwili ya siku?" Wanauliza watu wa mitaani.

Naam, nchi yetu imekumbwa na mafuriko ya habari. Kule bungeni Dodoma kuna moto unawaka. Zimeitishwa sanini 70 ili Jumatatu ipigwe kura ya kukosa imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Ndio, kuna wanaotaka Pinda ang'oke, na labda kutolewa kafara, maana, siamini kama tatizo la msingi ni Pinda, bali ni la kimfumo zaidi. Na jana kuna mbunge wa CCM kayasema makali yafuatayo;

“Mheshimiwa Naibu Spika, inashangaza na kusikitisha kuwa nchi inatafunwa. Wanaofanya haya ni mawaziri wetu. Nchi inakufa na tuelewe kuwa Tanzania sio mali ya CCM, ni ya Watanzania wote.“Mawaziri wetu wamekuwa mchwa, wanaangamiza nchi na leo nitamtaja waziri anayeongoza kwa kutafuta fedha za Watanzania. Ni Waziri wetu wa Fedha, Mustafa Mkulo. Ameuza viwanja, amelidanganya Bunge baada ya kuivunja CHC,”- Deo Filikunjombe ( CCM) Bungeni jana.

Lakini ya jana yalitanguliwa na ya juzi; Mbunge mwanadamizi wa CCM Godfrey Zambi aliyasema makali haya;

" CCM inaweza kung'olewa madarakani katika uchaguzi wa mwaka 2015 endapo kasi ya ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma itaendelea kama ilivyo sasa"- Godfrey Zambi ( CCM, Mbozi Mashariki).

Kauli za wabunge hao wawili wa CCM zinatoa tafsiri ya kilio cha wabunge wa CCM kuomba msaada kwa anayeweza kuwasaidia. Inatoa tafsiri pia kuwa hicho ni kilio cha wabunge wengi wa CCM. Kwamba hayo ndiyo wanayaongea hata chini chini.

Ndio, wananung'unika na wameanza kuiona adhabu wanayokwenda kuipata kutoka kwa wananchi ifikapo 2015. Wanaona pia, kuwa ' kisungura' hiki kidogo kinachopatikana kila mwaka kinavyoliwa na wajanja na wengine kuachiwa mifupa.

Wabunge wa CCM na wengine wanaona jinsi baadhi ya mawaziri wa kutoka chama chao wanavyojiangalia wenyewe kwa kujikatia zaidi kasungura hako kadogo na hata minofu mingine kuikimbizia kwenye majimbo yao badala ya kuangalia majimbo mengine pia. Hakika, Wabunge wa CCM sasa wanatoa kilio cha kuomba msaada na kilichochanganyika na hasira na hofu ya kupoteza mamlaka ya kuongoza dola ifikapo mwaka 2015. Ndio, kuna wanaokiona chama chao kikielekea kwenye kuzama 2015. Kelele wanazopiga bungeni zimegeuka kama kelele za nyikani, hazisikiki. Wameanza sasa kuwa na ujasiri wa kuzomeana wazi wazi kwenye vikao vyao badala ya kusubiri kuzomewa na wananchi hadharani. Naam, CCM ya sasa inapata tabu hata kwenye kujua namna ya kuitumia misamiati mipya ya kisiasa, maana, kuna wanaojivua gamba, wanaovuliwa magamba na sasa kuna ' wanaojinyambua' magamba wakiwa ndani ya chama- 'Political evolution' ya namna fulani.

Na Mtego wa Zitto Kabwe kwa CCM?

Jana Mbunge Zitto Kabwe ameitega CCM. Ni mtego wa hatari. Saini zile 70 zina maana hii;

- Kama wabunge wa CCM hawatachangamkia kutia sahihi zao zikavuka hata mia na hamsini, basi, kuna ujumbe unaopelekwa kwa umma. Kuwa wabunge wa CCM ni maneno tu, hawana dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi. Wabunge wengi wa CCM hawataiepuka adhabu ya umma inaweza kuwa inawasubiri 2015.

- Kwa wabunge wa CCM kutia sahihi zao na hata Pinda kupigiwa kura ya wabunge kukosa imani nae ina maana pia kuwa wabunge hawana imani na bwana mkubwa aliyemteua Pinda. Busara haiwataki wabunge wa CCM kufikia hapo. Hilo halina maslahi kwa taifa.

Nini kitakachotokea?

Kuna matatu;
Mosi, Mawaziri wale watano wanaotuhumiwa kwa ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma wanaweza kuepusha aibu kwa Serikali kwa wao wenyewe kutangaza kujiuzulu. Ingawa hili ni gumu kufanyika katika nchi hii, lakini, wakati mwingine kuna lazima ya kufanyika- maana, hapo watakuwa wamemnusuru Waziri Mkuu na aliyemteua.

Pili- Likishindikana la kwanza, basi, kabla ya Jumatatu, Waziri Mkuu Pinda awe ameshajiandaa kufanya maamuzi magumu. Kujiuzulu na kulinda heshima yake na ya aliyemteua. Au kutolewe ' Tamko la Serikali' litakalobadili upepo unaovuma sasa bungeni.

Tatu: La kwanza na la pili yaweza yasifanyike, na badala yake. Rais anaweza kuyaona yanayotokea sasa bungeni kama fursa ya kufanya mabadiliko makubwa Serikalini mara akitua Dar kutoka ziara ya Brazil.

Naam, yumkini pale Diamond Jubilee, kabla ya Jumatatu, kuna watakaopewa kazi ya kusafisha ukumbi na kupanga viti tayari kwa Mkuu wa Nchi kusema jambo kubwa kwa taifa kupitia kwa ' Wazee wa Darisalama'.

Na tusubiri tuone.

Maggid Mjengwa,

No comments: