Wednesday, April 11, 2012

Watu 200 waanguka kwa kuishiwa nguvu leo kwenye mazishi ya Kanumba

Na Ripota Wetu

ZAIDI ya watu 200 waliishiwa nguvu na kuanguka wakati wa mazishi muigizaji maarufu Steven Kanumba, miongoni mwao wakiwamo wasanii wawili maarufu nchini, Jackline Wolper na Wema Sepetu.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Slaam leo, Mwenyekiti wa Tiba na Kamati ya Mzishi Dk. Nassoro Ally alisema kuanguka kwa watu hao kumetokana na mkusanyiko mkubwa wa watu ambao ameulinganisha na ule ulijitokeza wakati wa mazishi ya Julius Nyerere.

Alisema hata hivyo, baadhi ya watu hao walioanguka wengi wao walipatiwa huduma ya kwanza akiwamo Wolper na watu wa Msalaba Mwekundu na kisha kuruhusiwa kuendelea na shughuli za mazishi za muigizaji huyo maarufu Barani Afrika.

Dk. Ally alisema hali hiyo,imekuwa ikijitokeza katika mikusanyiko ya namna ile ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya moyo, kukosa hewa ya kutosha na wengine kuanguka kutoka juu ya miti walikokuwa wamepanda kushuhudia tukio hilo.

Kwa upande wa muigizaji Wema Sepetu hali ilikuwa mbaya ukilinganisha na mwenzake Wolper kwani ilibidi akimbizwe katika hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu zaidi.

Baada ya kupata haafueni,Wema Sepetu aliongea na Ripota Wetu aliefika hospitalini hapi na akiwa kitandani  alisema alijisikia ghafla akiishiwa nguvu na kushindwa kujitambua na kujikuta akianguka na kupoteza fahamu.

Alisema hali hiyo imechangiwa na njaa kwani alifika katika maeneo viwanja vya Leaders akiwa hajapata hata kifungua kinywa, joto kali huku akizunguukwa na watu wengi kila alipokuwa akikaa.

Awali msemaji wa Hospitali hiyo ya Mwananyamala Edward Bisekala alisema hali yake siyo mbaya kama mnavyomuona akiwa na drip ambapo hali hiyo imesababishwa pressure.

Hadi Ripota Wetu anaondoka hospitalini hapo kulikuwa na watu wapatao wanne wakiwa wamewekewa drip ambapo pia hali zao hazikuwa mbaya.

Aidha, katika hatua nyingine baba mzazi wa muigizaji huyo, Mzee Charles Kanumba alisema malengo ya mwanaye kisiasa ilikuwa agombee ubunge mwaka 2015 kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kwa mujibu wa Redio Wapo Kanumba alimwambia baba yake nia yake hiyo ambapo alikubaliwa na kuambiwa kuwa hilo ni chaguo lake kwani ana haki ya kuamua anachokipenda.

Mzee Kanumba alisema mipango yake hiyo ilikuwa ikienda vizuri kwani wakazi baadhi ya vijana walikuwa wakimuunga mkono kutokana na nia yake hiyo.


Kwa hisani ya Blog ya Mtaa kwa mtaa 

No comments: