Ndugu zangu,
Kama mtego ule wa panya, tutafanya makosa makubwa kama kuna watakaodhani, kuwa haya ya watu kuchinjwa na kujeruhiwa na mapanga yatawakuta watu wa kundi fulani tu. Tukiacha yaendelee, basi, yeyote yule, bila kujali dini, rangi, itikadi au hata wadhifa wake, anaweza kuwa mhanga wa maovu haya. Kama taifa, kwa pamoja tuwalaani wauaji hawa na wanaowatuma.
Na kwa vyama vya siasa vilivyo makini na vinavyoitakia mema nchi yetu, vianze sasa kuachana na utamaduni wa kuwa na ‘wanamgambo’ ama vikundi vya vijana vinavyopewa mafunzo ya kijeshi kwa masuala ya ulinzi.
Historia inatufundisha,kuwa Afrika ‘ Parties militias’ ama vikundi vya wanamgambo vya vyama vya siasa huwa chanzo cha kuharakisha vurugu za kisiasa za wenyewe kwa wenyewe katika nchi na hata kupelekea mauaji. Tumeona Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kongo na kwengineko Afrika.
Ni vikundi hivi vya wanamgambo wa vyama ambavyo hutumika na vyama, wanasiasa, au hujituma vyenyewe kufanya kazi ya kulipiza visasi vya kisiasa kwa kutumia silaha.
Hapa kwetu tayari, vyama vikubwa vya siasa vina vikundi vya aina hiyo; CCM wana ‘ Green Guards’, Chadema wana ‘ Red Brigade’ na CUF wana ‘ Blue Guards’.
Katika nchi ya kisasa si busara kuwa na utaratibu unaoruhusu vyama vya siasa kuwa na vikundi kama hivyo vya vijana vyenye kupata mafunzo ya kijeshi.
Na hakika, Katiba yetu ijayo itusaidie kuondoa utaratibu kama huo wa ‘ kijima’ kwa kuweka marufuku ya vyama vya siasa kuunda vikosi vya vijana vyenye kukaa kambini na kupata mafunzo ya kijeshi, vikosi ambayo, vinaweza kuja kutumika vibaya na kutusababishia madhara makubwa kama taifa.
Kama vyama vitahitaji ulinzi kwenye shughuli zake, basi, viombe ulinzi kwenye makampuni ya ulinzi yanayotambulika kisheria na yasiyofungamana na siasa za vyama.
Vinginevyo, tuhakikishe jeshi letu la polisi linaimarishwa na linakuwa chombo cha usalama kinachoaminika na umma na kisichoegemea kwenye itikadi za vyama katika kufanya kazi yake. Vivyo hivyo, kwa vyombo vingine vya usalama katika nchi ikiwamo Idara ya Usalama wa Taifa. Vifanye kazi zao kwa kutanguliza maslahi ya taifa na si ya wanasiasa au vyama vyao. Inawezekana.
( Hii ni sehemu ya makala yangu kwenye gazeti la Mwananchi leo Jumapili)
Maggid Mjengwa
Iringa
0788 111 765
No comments:
Post a Comment