Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa chama hicho, Peter Kisumo
AMTAKA ABADILIKE ILI KUKINUSURU CHAMA,JK AZUIA HOJA YA ARUMERU
Midraj Ibrahim na Habel Chidawali, Dodoma
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama ameonywa akitakiwa kubadilika kwa sababu amekuwa mzigo.Taarifa kutoka ndani ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), zilieleza kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa chama hicho, Peter Kisumo ndiye alikuwa mchokozaji ambaye bila kumung’unya maneno alisema Mukama ameonyesha utendaji mbovu tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.Akijadili hali ya kisiasa nchini, Kisumo anadaiwa kumtuhumu Mukama kutumia muda mwingi kusema misamiati isiyokuwa na maana na faida kwa CCM.
“Unajua mzee (Peter Kisumo) alichana siyo kawaida, alimwambia Katibu kuwa ameshindwa kumaliza makundi, lakini amekuwa ni bingwa wa misamiati ambayo haina maana, amemwambia asipokuwa makini chama kinakwenda pabaya,” kilieleza chanzo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wakati Kisumo akishusha shutuma hizo, makofi mengi yalikuwa yakipigwa kuashiria kuungwa mkono na wajumbe wengi, lakini Mukama hakujibu chochote.
Pia, Mukama anadaiwa kushindwa kusimamia mikakati ya chama na makatibu wa CCM wakidaiwa kuwa wamekuwa dhaifu na hawana mipango mikakati ya kupambana na upinzani.
Kisumo alidai kuwa Mukama ameshindwa kuonyesha kama chama kinapanda kwenye duru za chini, huku akipendekeza pande zote zinazohasimiana ndani ya CCM kukaa pamoja na kuondoa tofauti zao ili kukinusuru.
“Ingawa hakufikia tamati, wajumbe wamemwelewa vizuri. Ametaka pande zinazohusika zikae, zielewane na zipendane ili kunusuru chama kwenye chaguzi,” kilidokeza chanzo chetu.
Hatua ya Kisumo kushambulia utendaji wa uongozi wa CCM ambao unasimamiwa na Mukama, inaonekana kuunga mkono kauli ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kuwa tatizo la CCM ni uongozi.
Lowassa aliwaambia wananchi katika mkutano wa hadhara huko Mtu wa Mbu Arusha kuwa CCM kinakabiliwa na matatizo ya kiutendaji na uongozi, lakini kuna mambo matano yanayomfanya aendee kuwa mwanachama wake.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni muundo mzuri wa chama, kutetea wanyonge, kudumisha umoja na mshikamano, kuwalinda raia wa kawaida katika kupata na kufaidi rasilimali za nchi dhidi ya matajiri na wawekezaji wa nje na mfumo mzuri unaowezesha watu kujisahihisha na kusema kuwa kitakapoacha misingi yake ya awali ikiwemo kutetea wanyonge, hatakuwa mmoja wa wanachama wake.
“Pamoja na uzuri wake, muundo wa chama chetu ni mzuri sana, imani ya chama chetu ni nzuri sana, misingi inayoongoza chama chetu ni mizuri sana, lakini tuna tatizo la utendaji na uongozi ndani ya chama chetu …ama katika kufanya uamuzi au uamuzi usio sahihi au kutochukua hatua kwa matatizo yanayowakabili wananchi kwa wakati muafaka. Tukionekana hatujali shida za wananchi wetu, watatafuta mbadala , lakini kero hizi zishughulikiwe kwenye vikao.”
Hata hivyo, Mukama alimjibu siku moja baadaye akisema haikuwa sahihi kwa Lowassa kutoa kauli hiyo kwenye mikutano ya hadhara wakati anajua bayana taratibu za chama hicho.Alisema alipaswa kuzungumzia matatizo ya jimbo lake yakiwemo migogoro ya ardhi, wawekezaji na wananchi, wakulima na wafugaji, maji na kero nyingine mbalimbali na si kukishambulia CCM.
Kauli hiyo ya Lowassa iliungwa mkono na mshirika wake kisiasa, James Ole Millya ambaye amejiunga Chadema hivi karibuni akisema tatizo jingine linalokikabili chama hicho tawala ni makundi.
Mbali ya Ole Millya, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Ruben Olekuney naye alimkosoa Mukama akisema amekurupuka kumjibu Lowassa akisema Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu, alikuwa akizungumzia uongozi wa chama hicho eneo la Mto wa Mbu na si wilaya, mkoa au taifa.
“Katika ziara tuliyofanya na Mh Lowassa Mto wa Mbu, kero nyingi ziliibuka na kero hizo zilikwishapelekwa kwenye ngazi ya kata lakini, hazikushughulikiwa na wanachama wakatishia kukihama chama kwani kero zao hazijashughulikiwa,” alisema na kuongeza kuwa hali ilikuwa tete kwa upande wa CCM eneo hilo la Mto wa Mbu.
Aliongeza: “Unajua watu wanamuamini na kumpenda huyu mzee sasa tulipokwenda pale tukakubaliana kuchukua uamuzi wa haraka na kweli ikasaidia, ndipo katika mkutano ule Edward (Lowassa) akasema kuna tatizo la uongozi kwenye chama, lakini chama ni kizuri akimaanisha chama ngazi ya kata ile.”
“Kwa kweli Mzee Mukama anatakiwa kwanza asome ‘content’ (maudhui) ya yale aliyosema Edward siyo kukurupuka, huku kwenye ngazi ya chini kuna matatizo makubwa ya uongozi. Kwanza alitakiwa aje kusaidiana nasi kukabiliana na kasi ya Chadema na siyo kukurupuka,” alisisitiza.
Mwenyekiti huyo wa CCM Monduli alisisitiza kuwa mbunge huyo wa Monduli katika ziara yake hiyo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutuliza kasi ya upepo wa wanaCCM kukimbilia upinzani.
“Hii kazi ilitakiwa ifanywe na kina Mzee Mukama, sasa Edward sielewi wanamshutumu kwa lipi wakati amekuja kuimarisha uhai wa chama. Si aulize kwanza kuliko kukurupuka tu magazetini?”
Hoja ya Arumeru
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinadai kwamba Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alilazimika kuingilia kati kuokoa sekretarieti kutuhumiwa kuhujumu mgombea ubunge wa CCM kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki.
Vyanzo vyetu ndani ya kikao hicho, vilidai kuwa hoja ya uchaguzi wa Arumeru Mashariki iliondolewa na Rais Kikwete akielekeza irejeshwe Kamati Kuu hatua inayodaiwa kuwa ililenga kuokoa sekretarieti ya chama hicho iliyokuwa imepaniwa na wajumbe kutaka iwajibishwe.
Sekretarieti hiyo inatuhumiwa kuhujumu uchaguzi wa Arumeru na kwamba ilikuwa ikishiriki kumchafua mgombea wa CCM, Sioi Sumari.
Chanzo chetu kilidokeza kuwa, walipanga kupendekeza Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Katibu wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Mchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, wapewe karipio kali kutokana na kuhujumu chama Arumeru.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangoye alisimama kutaka kuchangia hoja hiyo lakini alizuiwa na Rais Kikwete huku akielekeza irejeshwe Kamati Kuu kujadiliwa.
Chateua makatibu wa mikoa
Chama hicho kimeunda mkoa maalumu wa vyuo vikuu na kuthibitisha uteuzi wa makatibu wa mikoa.
Nape alisema jana mjini hapa kwamba chama kimeamua kufanya hivyo ili kukidhi matakwa ya vijana wa CCM walioko kwenye vyuo mbalimbali nchini.
“Kuundwa kwa mkoa maalumu wa wanafunzi wa elimu ya juu, kunalenga kupanua wigo ikiwa ni mkakati wa chama kujiimarisha zaidi kwa wanachama wake wa kada mbalimbali, watapata nafasi ya kushauri na kushiriki moja kwa moja uamuzi wa ngazi ya juu katika CCM,” alisema Nape.
Makatibu walioteuliwa na mikoa yao kwenye mabano, ni Elikana Mauma (Mara), Hilda Kapaya (Geita), Shaibu Akwilombe (Simiyu), Hosea Mpagile (Njombe) na Alphonce Kinamhala (Katavi).
Wengine ni Aziza Mapuri (Mkoa wa Magharibi), Christopher Ngubiagai (Mkoa wa Vyuo Vikuu) na Adelina Geffi na Maganga Sengerema ambao watapangiwa vituo vya kazi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment