Kampuni ya umeme Tanzania (Tanesco) imetoa mikakati yake juu ya uboreshaji wa umeme nchini ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Afisa Mchambuzi wa Maswala ya Fedha wa kampuni hiyo ndugu Mathew Maduhu katika maadhimisho yanayoendelea ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika viwanja vya Mnazi mmoja.
Bwana Maduhu amesema mikakati hiyo ni ile ya muda mfupi ya kati na ile ya muda mrefu,ambapo mikakati ya muda mfupi ni ujenzi wa mitambo ya MW 100 Ubungo jijini Dar es salaam ambao utakuwa unatumia gesi asili,
Alitaja mipango mingine ni pamoja na ujenzi wa mitambo ya MW 60 eneo la Nyakato mkoani Mwanza na kununua umeme wa kampuni ya Symbion Power wenye uwezo wa MW 100.
Mikakati mingine ni pamoja na mradi wa Kinyerezi wa MW 240 unatumia gesi ya asili , Mradi wa Kiwira wa MW 200 ambao unatumia makaa ya mawe na mradi wa umeme wa Singida wa MW 50 unaotumia nguvu ya upepo.
Aidha Bwana Maduhu ametaja baadhi ya mikakati ya muda mrefu kuwa ni ile ya mradi wa Songwe Mbeya wa MW 650 unaotumia joto ardhi ,mradi wa Mchuchuma wa MW 600 unaotumia makaa ya mawe na miradi ya Ngaku wa MW 400 unaotumia makaa ya mawe.
Naye Mjiolojia Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ndugu Habass Ng’ulilapi ameeleza kuwa utekelezaji wa mkakati huuo unahitaji fedha za kutosha hadi ukamilike , na kuisisitiza serikali itupie macho suala hilo ili kufanikisha mkakati huo.
Aidha bwana Habass amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia wananchi kuepukana na adha ya tatizo la umeme nchini.
No comments:
Post a Comment