Wednesday, July 27, 2011

WAMA na FHI pamoja tuwalee wa waanza kufanya kazi ya kuwakomboa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi

Afisa Tathimini na Ufuatiliaji kutoka Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Gloria Minja akiwaelezea wajumbe wa mradi wa kuwakomboa watoto wa kitanzania wanaoishi katika mazingira hatarishi jinsi mradi huo unavyofanya kazi katika wilaya 25 hapa nchini. WAMA kwa kushirikiana na Family Health International (FHI) Pamoja Tuwalee wamedhamiria kuhakikisha kuwa watoto hao wanapata elimu na kuishi maisha mazuri kama walivyo watoto wengeni.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya wadau mbalimbali wa mradi wa kuwakomboa watoto wa kitanzania wanaoishi katika mazingira hatarishi wakimsikiliza Afisa Tathimini na Ufuatiliaji kutoka Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Gloria Minja (hayupo pichani) wakati akiwaelezea umuhimu wa mradi huo ambao utafanya kazi katika wilaya 25 hapa nchini. WAMA kwa kushirikiana na Family Health International (FHI) Pamoja Tuwalee wamedhamiria kuhakikisha kuwa watoto hao wanapata elimu na kuishi maisha mazuri kama walivyo watoto wengeni.

Wajumbe wa kamati ya wadau mbalimbali ya kuwakomboa watoto wa kitanzania wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa wadau hao uliofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Grand Villa iliyopo jijini Dar es Salaam.Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwa kushirikiana na Family Health International (FHI) Pamoja Tuwalee wameshaanza kufanya kazi katika wilaya 25 hapa nchini.


Na Anna Nkinda – Maelezo

Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwa kushirikiana na Family Health International (FHI) Pamoja Tuwalee wameanza kufanya kazi katika wilaya 25 hapa nchini ya kuwakomboa watoto wa kitanzania wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kuunda kamati mbili ambazo zitatengeneza na kusimamia kampeni za ushauri na utetezi kwa watoto hao.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Gloria Minja ambaye ni Afisa Tathimini na ufuatiliaji wa WAMA wakati akiongea na wajumbe wa kamati hizo ambazo ni kamati ya watoto wanaotoka katika mazingira hatarishi na kamati ya wadau mbalimbali katika ukumbi wa mikutano wa Grand Villa jijini Dar es Salaam.

Alilifafanua kuwa katika kamati ya watoto wanaotoka katika mazingira hatarishi itakuwa na wajumbe sita na kamati ya wadau mbalimbali itakuwa na wajumbe nane kutoka Serikali kuu ambayo ni wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii , halmashauri za wilaya, manispaa na miji, Asasi za Kiraia, vyombo vya habari, sekta binafsi na wafanyakazi wa WAMA na FHI.

Minja alisema kwamba lengo kubwa la mradi huo ni kuboresha hali ya maisha ya watoto wanaotoka katika mazingira hatarishi hasa watoto wa kike na kaya zao kwa kuwajengea uwezo wanakaya na jamii ili watoe huduma kamilifu, bora na endelevu kwa watoto hao na utakuwa tofauti na miradi mingine ambayo inashughulika na mtoto.

“Kwa mfano watoto wengi wanaoishi katika mazingira hatarishi wanashindwa kwenda shule kutokana na ukosefu wa chakula kwenye kaya zao hivyo basi wanalazimika kwenda kutafuta fedha za kununua chakula bali katika mradi huo kaya anayotoka mtoto itapata chakula ili mtoto aweze kwenda shule”, alisema Minja.

Alimalizia kwa kusema kuwa wajumbe wa mradi huo wataweza kufahamu mradi wa pamoja tuwalee jinsi unavyofanya kazi na mipango ya kampeni za ushawishi na utetezi kwa watoto wanaishi katika mazingira hatarishi.

Akiongea kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo Christopher Mushi kutoka wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto alisema kuwa wanafanya kazi kwa kujituma, kujitolea na uaminifu kutokana na hadidu za rejea zilizoandaliwa na wajumbe husika ili kuhakikisha kuwa kampeni hiyo inakuwa yenye mafanikio.

Naye Jesse Orgenes mjumbe kutoka FHI Pamoja Tuwalee alisema kuwa mradi huo ni mzuri na umekuja kwa wakati muafaka kwani hivi sasa kuna ongezeko kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi waliopo mitaani ambao wanahangaika kutafuta fedha badala ya kwenda shule kupata elimu.

“ Hivi sasa hatutakiwi kuendelea kutegemea wafadhili kutoka nje ya nchi ambao watawasaidia watoto hawa kinachotakiwa ni jamii nzima kufanya kazi kwa pamoja ya kuwasaidia watoto hawa”,alisema.

Pamoja Tuwalee ni mradi wa miaka mitano na unafadhiliwa na Serikali ya Mrekani kupitia ofisi ya shirika lao la Maendeleo hapa nchini (USAID Mission/Tanzania) mradi huo unafanya kazi kazi katika mikoa ya Dar es Salaam wilaya tatu, Pwani wilaya sita, Morogoro wilaya sita na Zanzibar wilaya 10.

No comments: