Thursday, July 28, 2011

Wanasheria waomba mabosi Dowans washitakiwe


KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimewasilisha ombi Mahakama Kuu kutaka wakurugenzi wa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans wapandishwe kizimbani kwa kudharau amri ya Mahakama. Ombi hilo liliwasilishwa jana na Wakili wa kituo hicho, Dk. Sengodo Mvungi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kupangiwa tarehe za kutolewa kwa uamuzi wa pingamizi lao kuzuia Serikali kuilipa kampuni hiyo fidia ya Sh bilioni 94. Kuwasilishwa kwa ombi hilo kunatokana na taarifa zilizoripotiwa kwenye magazeti kuwa Dowans imeuza mitambo yake kwa Kampuni ya Symbion Power ya Marekani jambo ambalo Dk. Mvungi alidai ni kinyume na amri iliyotolewa na Mahakama. Katika amri hiyo iliyotolewa Machi 2 mwaka huu, iwapo upande wowote ungehitaji kufanya lolote ni lazima waombe kibali cha Mahakama. LHR ni moja kati ya mashirika matatu yanayopinga kusajiliwa kwa Tuzo ya Dowans ya Sh bilioni 94 iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (1CC). Dk. Mvungi alidai kuwa, wakurugenzi hao wamekiuka amri hiyo na wanastahili kufika mahakamani kujitetea, na kuwa habari za kuuzwa kwa mitambo hiyo ziliripotiwa na magazeti zaidi ya sita na ameshaandaa kiapo cha suala hilo. Kwa upande wake Mwandishi wa Habari, Timoth Kahoho ambaye pia anapinga jambo hilo alidai kuwa ombi hilo ni muhimu kwa kuwa mitambo iliyouzwa ndio sababu ya mgogoro huo na imesababisha wote wafike mahakamani kupinga. Hata hivyo Wakili Lugano Mwandambo aliyekuwa anamuwakilisha wakili wa Dowans, Kenedy Fungamtama alidai hawezi kujadili suala ambalo hana maelekezo nalo na kuomba asizungumzie lolote mpaka Fungamtama atakapofika. Jaji Emilian Mushi alisema, Mahakama haiwezi kusikiliza ombi hilo mpaka itakapotoa uamuzi wa mapingamizi mawili yaliyowasilishwa mahakamani hapo na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 11 mwaka huu kwa ajili ya kupanga tarehe ya kutoa uamuzi wa mapingamizi hayo. Awali Naibu Mwanasheria wa Serikali, George Masaju alidai kuwa, Dowans wamefungua kesi nyingine katika Mahakama Kuu ya Uingereza na uamuzi wa shauri hilo unatarajiwa kutolewa Novemba 20 mwaka huu. Hata hivyo Jaji Mushi alisema shauri hilo haliwezi kuzuia mwenendo wa kesi hiyo. Novemba 15, mwaka jana Mahakama ya ICC chini ya Mwenyekiti Gerald Aksen na wasuluhishi, Swithin Munyantwali na Jonathan Parker iliamuru Shirika la Umeme (TANESCO) kuilipa Dowans fidia ya Sh bilioni 94 kwa kuvunja mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha sheria. Baada ya uamuzi huo, Januari 25 mwaka huu Dowans iliwasilisha mahakamani hapo ombi la usajili wa tuzo hiyo ili ulipwaji wa fidia yake ufanyike kisheria na siku chache baadaye LHRC, Kahoho na mashirika mengine ya Leat na Sikika waliwasilisha ombi la kutaka tuzo hiyo isisajiliwe.


Chanzo: Habari Leo

No comments: