Saturday, September 10, 2011

RAIS DKT JAKAYA KIKWETE ATUMA SALAM ZA RAMBI RAMBI VIFO VYA ABIRIA WA MELI ZANZIBAR


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kuomboleza msiba mkubwa wa vifo vya mamia ya watu waliopoteza maisha yao katika ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Spice Islander usiku wa kuamkia leo, Jumamosi, Septemba 10, 2011 katika Bahari ya Hindi ambapo watu zaidi ya 170 wanaripotiwa kufa maji.

Katika salamu hizo, Mheshimiwa Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshtuko, masikitiko na huzuni kubwa taarifa ya ajali na kuzama kwa meli ya Mv Spice Islander, usiku wa kuamkia leo, tarehe 10, Septemba, 2011. Kutokana na kuzama huko, abiria wengi wamepoteza maisha na wale walionusurika wamepata athari mbalimbali zifanyazo afya zao kuhitaji uangalizi wa karibu. Aidha mali nyingi zimeteketea.”

“Haya ni maafa makubwa kwa nchi yetu na Watanzania wote wako pamoja na ndugu zao wa Unguja na Pemba katika kipindi hiki kigumu. Kwa niaba yao nakutumia salamu za mkono wa pole na kupitia kwako naomba unifikishie salamu za rambirambi kwa ndugu zetu waliopoteza ndugu na jamaa zao. Nawaomba wafahamu kuwa msiba wao ni msiba wetu sote, majonzi yao ni majonzi yetu na uchungu wao ni uchungu wetu sote. Tunawaombea wawe na moyo wa subira na uvumilivu na tunaungana nao kuwaombea marehemu wetu kwa Mola awape mapumziko mema, awasamehe madhambi yao na kuwajaalia pepo,” amesema Mheshimiwa Rais na kuongeza:

“Kwa ndugu zetu walionusurika katika ajali hiyo, tunawapa pole kwa msukosuko mkubwa walioupata. Tunaungana nao kumshukuru Mwenyezi Mungu kuokoa maisha yao na tunawaombea wapone upesi ili waweze kuendelea na juhudi za kujiletea maendeleo yao na kuijenga nchi yetu.”

Amehitimisha Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete: “Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nakuhakikishia ushirikiano wangu binafsi na ule wa wenzetu wote katika hatua zote za kukabiliana na janga hili na athari zake. Tutakupa kila aina ya msaada utakaohitaji tutoe.”






No comments: