Tuesday, September 13, 2011

SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZA NAIBU KATIBU MKUU UMOJA WA MATAIFA

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro akisaini kitambu cha maombolezo kilichofunguliwa katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa, kufuatia ajali ya kuzama kwa meli MV Spice Islander.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro akipeana mkono wa pole na Mhe. Ombeni Sefue, Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro amewatumia salamu za pole Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV Spice Islander iliyotokea tarehe 10 Septemba 2011.

Katika salamu zake kwa viongozi hao pamoja na watanzania wote, Dkt. Migiro anasema ameshtushwa na kusikitishwa sana na taarifa za ajali hiyo. Hata hivyo ameguswa na kupata faraja kubwa mno, kwa namna ambavyo serikali hizo mbili, na kwa kushirikiana na wananchi wake zilivyoweza kuratibu na kusimamia zoezi zima la ukoaji wa abiria walionusurika na uopoaji wa miili ya marehemu.

Naibu Katibu Mkuu anasema,kama alivyosema Katibu Mkuu Ban ki Moon katika salamu zake kwamba, Umoja wa Mataifa upo pamoja na watanzania katika kipindi hiki kigumu. Aidha Dkt, Asha-Rose Migoro anasema dua na sala zake anazielekeza kwa waathirika na familia zao, na anawatakia nafuu ya haraka majeruhi wote.

IMETOLEWA NA UBALOZI WA TANZANIA UMOJA WA MATAIFA


No comments: