Monday, October 3, 2011

CCM IRINGA YAREJESHA HESHIMA YAKE


Katibu wa CCM mkoa wa Iringa Mary Tesha


Wabunge wa Chadema mkoa wa Iringa Mchungaji Peter Msigwa (kulia) ,Chiku Abwao na aliyekuwa mgombea udiwani kata ya Kitanzini Gervas Kalolo pamoja na katibu wa Chadema wilaya ya Iringa mjini Suzana Mgonokulima siku ya kuchukua fomu


Diwani mteule Nicolina Lulandala (kulia) siku ya kuchukua fomu ya kuwania udiwani Gangilonga


Jesca Msambatavangu diwani mteule Kitanzini (kulia)


Na Francis Godwin
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kifanikiwa kulinda heshima yake kwa kumpata mrithi wake katika kata zote tatu za mkoa wa Iringa kwa kuiadhibu Chadema .




Katika kata ya mji Mwema Jimbo la Njombe kusini mgombea wa CCM Jimy Ngumbuka alishinda kwa kura 743 kati ya kura 508 .




Huku katika jimbo la Iringa mjini kata zote mbili ya Gangilonga na Kitanzini CCM ikiibuka na ushindi wa kishindo dhidi ya vyama vya upinzani .


Kwa mujibu wa msimamizi msaidizi wa uchaguzi Jimbo la Iringa mjini, Martin Ndamo CCM wamefanikiwa kutetea kata zote mbili walizokuwa wakiziongoza tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliopita huku Chadema ikiambulia nafasi ya pili katika kata zote




Alisema katika uchaguzi huo mgombea wa CCM, Kata ya Miyomboni/Kitanzini, Jesca Msambatavangu aliibuka mshindi kwa kupata kura 647, akifuatiwa na Mgombea wa Chadema Gervas Kalolo ambaye alipata kura 571, huku mgombea wa CUF, Ahmed Lyelu wa CUF na Nasir Mpeta wa NCCR-Mageuzi wakiambulia kura mbili kila mmoja.


Ndamo alisema katika Kata ya Gangilonga, Nicolina Lulandala (CCM) ameibuka mshindi kwa kuwamwaga wapinzani wake baada ya kupata ushindi wa kura 501, Edwin Sambala (Chadema) kura 308 na mgombea wa NCCR-Mageuzi Karrim Masasi kura nne.


Uchaguzi huo ulikuwa ukifanyika kwa ajili ya kujaza nafasi zilizoachwa wazi na Abubakari Mtamike (CCM)aliyefariki dunia mwishoni mwa mwaka jana na Mariam Nyanginywa(CCM) aliyefariki mwanzoni mwa mwaka huu,ulivihusisha vyama vinne vya CCM,Chadema,CUF na NCCR-Mageuzi.


Katibu wa CCM mkoa wa Iringa, Mary Tesha alisema kuwa, ushindi huo umetokana utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama hicho tangu walipoingia madarakani mwaka jana licha ya kukubali kuwa, mwaka huu walipata changamoto kubwa kutoka kwa wapinzania wao.


Alisema ukweli ni kwamba, CCM wamerejesha maeneo ambayo walikuwa wakiongoza tangu awali na kwamba kilichopo ni kwa Chadema kujipanga upya ikiwemo ukitoa elimu ya Uraia kwa wananchi kujua haki zao, ikiwemo kujiandikisha kupiga kura na kupiga kura yenyewe.


Katibu wa Chadema wilaya ya Iringa mjini Suzana Mgonokulima alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi juu ya matokeo hayo alisema kuwa atayatolea ufafanuzi zaidi kesho

No comments: