Wednesday, October 26, 2011

KATIBU MKUU WA UVCCM ALAANI KITENDO CHA KADA WAO KUMWAGIWA TINDIKALI

Kijana Musa Tesha aliemwagiwa tindikali wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga mkaoni Tabora,akiwasimulia waheshimiwa,Katibu Mkuu wa UVCCM,Martin Shigela (kushoto) na Mbunge wa Viti maalum kupitia UVCCM mkoani Arusha,Catherine Magige (kulia) jinsi tukio halisi lilivyo mtokea.

Na Woinde Shizza,Moshi

BAADHI ya Vijana wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) wa Mjini Igunga waliohusika na kitendo cha kumwagia tindikali kijana mmoja ambaye ni mfuasi wa chama cha mapinduzi wamelaaniwa vikali na katibu mkuu wa Umoja wa vijana wa CCM(UVCCM) Taifa Martine Shigela kwa kufanya kitendo hicho cha kinyama na chakiuuwaji na kusema kuwa kufanya hivyo sio siasa bali ni upuuzi .


Katibu Mkuu huyo alilaani kitendo hicho mara baada ya kumuona kijana huyo ambaye kwa sasa yupo mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya matibabu ya jeraha hilo ambalo analo katika paji lake la uso pamoja na mkono na kusema kuwa waliousika na tukio hilo wamelaaniwa hadi kwa mungu.

Katibu huyo aliyasema hayo jana mjini hapa wakati alipomtembelea Musa Tesha(24) mkazi wa Igunga ambaye alikuwa anapatiwa Matibabu katika hospitali ya Rufaa ya KCMC baada ya kumwagiwa tindikali na wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA),kwenye uzinduzi wa Kampeni za uchaguzi huo.

“Kwakweli nimehuzunishwa sana na vijana hawa waliohusika na kitendo hiki kwani ni cha kinyama kabisa,kweli unamwagia binadamu mwenzako tindikali unamuaribu kisa chama jamani mbona waliohusika na kitendo hichi wamekosa ubinadamu sasa kama wameanza kufanya siasa za hivi mapema hii huko tunapoenda sindio balaa"alisema Shigela

Alibainisha kuwa ni jambo la kulaani kwa yeyote mpenda amani,inasikitisha pale ambapo vijana wanatumika na vyama vya siasa kuharibu maisha ya wenzao.

Shigela aliwataka vijana kuhakikisha kuwa wanashirikiana katika mambo ya msingi na kuwa na ushirikiano ili kuweza kujenga taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Arusha James Ole Millya ambaye alikuwa ameongozana na Katibu huyo akizungumzia tukio hilo akisema kuwa kitendo hicho ni cha unyama na sio kizuri kwani watu wanakosa ubinadamu kwa sababu ya chama alisema kuwa Tanzania nchi ambayo inaamani haitakiwi kuwa hivyo kwani hata katika historia yake uko nyuma haikua hivyo.

"huu ni unyama usiovumilika siasa zisitufikishe mahali ambapo mtu anaweza kutoa roho ya mwenzake kwa sababu ya siasa,wanasiasa tunatakiwa kushawishiana kwa hoja,hatuwezi tukagombania fito moja wakati sisi wote ni Watanzania na tunajenga nyumba moja”alisema Millya

Akizungumzia tukio hilo Musa ambaye ni Mkazi wa wilayani Igunga mkoani Tabora,alisema kuwa siku ya tukio akiwa anabandika mabango ya Mgombea wa kiti cha ubunge kwa tiketi ya CCM,ghafla walitokea wafuasi wa Chadema na kumkamata wakidai kuwa wanampeleka polisi.

Alidai kuwa siku ya tukio Sepemba 6 mwaka huu,vijana hao ambao walikuwa ni wa Igunga Mjini,badala ya kumpeleka polisi kama walivyokuwa wamemweleza,walimpeleka katika kichaka kidogo ambapo walimvamia na kummwagia tindikali usoni na katika mkono wake wa kulia.

"walinipeleka porini kisha wakanimwagia tindikali na kunipiga sasa baada ya kufanya vile nilijitaidi kujisogeza hadi eneo la nyumba za watu na kwa bahati nzuri nikakuta nyumba moja karibu na pale nikagonga nao wakanisaidi wakatoa taarifa na nikasaidiwa kwakweli nawashukuru sana wale ambao wamenisaidia mpaka sasa na pia nashukuru sana chama kinavyonisaidia na pia nyie mliokuja kunitembelea nawashukuru kwani jinsi mnavyokuaja mnazidi kunitia moyo"alisema Musa

Aidha baada ya kijana huyo kumwagiwa tindikali alipatiwa msaada na wananchi waliokuwa karibu na eneo hilo,ambapo aliletwa mjini hapa kwa ajili ya matibabu katika hospitali ya Rufaa ya KCMC,ambapo CCM inagharamia gharama za matibabu yake.

Kwa sasa hali ya kijana huyo inaendelea vizuri ambapo jana aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo huku akiendelea kupatiwa matibabu nyumbani kwa baba yake mdogo huku jicho la kulia likiwa halijafunguka huku lakushoto likiwa limefunguka na linaona kidogo japo kuwa bado linatiririsha machozi.

Naye Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Arusha kupitia umoja wa vijana (UVCCM) Catherini Magige alisema kuwa amesikitishwa sana na tukio hilo la kijana huyo aliyemwagiwa tindikali.

"unajua sisi ni watu wa baba mmoja kama ni mafundi tunajenga nyumba moja sasa kama tunajenga nyumba moja yanini kugombania fito za kujengea wakati nyumba ni moja tunajenga eeh jamani vijana wa kitanzania hatutakiwi kugombana hatutakiwi kutoana roho kwa ajili ya chama kimoja au kingine tunachotakiwa kufanya ni kukaa na kujadiliana na kuelimishana jinsi ya kujenga nchi yetu na sio kuvurugana"alisema Magige.

Kufuatia tukio hilo Katibu wa UVCCM taifa aliahidi kiasi cha shilingi milioni 5 kutoka katika Jumuiya hiyo pamoja na kumpatia mtaji wa biashara kijana huyo pindi atakapo pona na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Arusha kupitia(UVCCM) alimuahaidi kumpatia shilingi milioni moja za kumsogeza na kumsaidia pindi atakapo pona.

No comments: