NA FAKI MJAKA-MAELEZO ZANZIBAR
Makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Serikali ya Zanzibar kwa kushirikiana na India zimefanya makubaliano ya awali ambayo yatapelekea India kujenga viwanda, Shule na Vyuo Zanzibar.
Maalim Seif ameyasema hayo jana jioni katika mkutano na waandishi wa habari Uwanja wa Ndege wa Karume Zanzibar mara tu alipowasili kutoka ziara ya kikazi Nchini India.
Amesema katika ziara hiyo India imeonesha nia ya kuisaidia Zanzibar katika nyanja mbali mbali ikiwemo Kilimo, Elimu, Teknolojia ya Mawasiliano, Uvuvi na Biashara.
Katika upaande wa kilimo amesema wazanzibari watapata fursa ya kwenda India kwa ajili ya kujifunza shughuli za kilimo ikiwemo utafiti wa mbegu, udogo na mbolea ambapo nchi hiyo imepiga hatua kubwa.
Amesema kuwa wataalamu wa kilimo nchini India wanawafikia wakulima kwa kuwapa taaluma mbalimbali zikiwemo utengenezaji wa teknolojia rahisi ya kutumia mbolea ambayo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji.
Aidha amesema India imeweza kupiga hatua katika kilimo kutokana na Serikali yake kuwajali wakulima kwa kuwapa mikopo wakulima ambao wamejiunga katika vikundi vya ushirika.
Akiielezea shughuli za uvuvi Makamo huyo wa kwanza wa Rais amesema India imeweza kuwasajili wavuvi wote na kuwapatia zana muhimu kama vile boti zenye mawasiliano jambo ambalo ni muhimu pale inapotokea maafa.
Aidha amesema kilimo cha samaki kimeweza kupiga hatua kutokana na utaalamu unaotumika katika uzalishaji wa mbegu bora za samaki ambazo utafiti unapokamilika mbegu hizo husambazwa kwa wakulima wa samaki.
Akiwa nchini Dubai Maalim Seif alikutana na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza Zanzibar na kumuhakikishia kuwa wako tayari ndani ya wiki mbili kuja Zanzibar kwa ajili ya kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu.
Aidha wawekezaji hao kutoka Dubai wameahidi kuwekeza katika sekta ya afya kwa kujenga hospitali kubwa mbili za kisasa moja Unguja na nyengine Pemba.
Wawekezaji hao pia wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuandaa miundo mbinu bora ambayo itarahisisha utekelezaji wa miradi hiyo kwa maendeleo ya Zanzibar.
Katika ziara hiyo ya kiserikali Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif alifuatana na Waziri wa Elimu,Waziri wa Biashara pamoja na Maofisa mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment