Wednesday, October 5, 2011

MKUU WA MKOA WA RUKWA AANZA KUCHUKUA HATUA KUKABILIANA NA HALI MBAYA YA VYOO VYA SHULE ZA MSINGI MKOANI HUMO


Ni taarifa iliyowasilishwa na Kikosi Kazi alichounda Mkuu wa Mkoa aliyemaliza muda wake Bw. Daniel Ole Njoolay ndiyo iliyoibua hali halisi ya vyoo vya shule ya msingi katika Mkoa wa Rukwa.

Taarifa hiyo iliwasilishwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Bi. Catherine Mashalla kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) tarehe 29 Septemba 2011 katika ukumbi wa RDC Wilayani Sumbawanga.



Taarifa hiyo ilionyesha kuwa katika shule zote 515 za msingi mkoani Rukwa zenye jumla ya wanafunzi 285,486 zina mahitaji ya matundu ya vyoo 12,956 kukidhi mahitaji ya wanafunzi hao ambapo tundu moja linawiana na wanafunzi 25 kwa wavulana na 20 kwa wasichana.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo matundu yaliyopo ni 5523 sawa na asilimia 43% ya utoshelevu, matundu 7745 ni pungufu. Aidha vyoo vingi vilivyopo havina ubora unaokidhi hali iliyopelekea uongozi wa mkoa kuipokea taarifa hiyo kama changamoto na kuanza kuchukua hatua kuondokana na tatizo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya (MB) aliipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili nakusema "tumeshajitathmini kinachofuata sasa ni kuandaa mikakati mbadala ya kuweza kutatua tatizo hili".

Miongoni mwa hatua zilizoanza kuchukuliwa ni pamoja na Mkuu huyo wa mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya (MB) kuchagua shule ya mfano itakayojegwa vyoo bora na ifikapo tarehe 09 Desemba 2011 kwenye kilele cha maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara itakabidhiwa ikiwa imekamilika. Shule ya Msingi Mbarika ndiyo iliyochaguliwa ambayo ipo katika manispaa ya Sumbawanga.
Hatua nyingine ni uchangishaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyoo bora ambapo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alianza harambee hiyo kwa kutoa shilingi laki 5, huku akitoa laki 3 taslim na laki 2 ikiwa ni ahadi.
Uchangishaji huo wa fedha ulifanyika katika ukumbi wa Upendo uliopo katika wilaya ya Sumbawanga katika hafla ya kuwapongeza wajasiriamali wa Mkoa wa Rukwa walioshinda katika maonyesho ya Nanenane yalifanykia kikanda mkoani Mbeya.

Jumla ya fedha zilizochangishwa katika harambee hiyo ni zaidi ya shilingi milioni 2.1, na miche 100 ya miti itakayopandwa wakati wa masika katika shule ya Msingi Mbarika iliyoahidiwa na mmoja wa wadau wa mazingira.

Katika hatua nyingine ya kukabiliana na tatizo hilo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amemuagiza mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga kufuatilia kwa karibu ujenzi na ukarabati wa vyoo katika shule ya mfano iliyoteuliwa ya Mbarika na kumtaka kushirikiana na watendaji na uongozi wa shule kuitisha kikao cha wazazi ili nao kila mmoja achangie shilingi alfu 3 kwa ajili ya ujenzi huo.

Huo ni mwanzo tu wa mpango wa kuboresha huduma ya vyoo katika shule za Mkoa wa Rukwa, utaratibu wa kuboresha vyoo utaendelea hadi kuenea Mkoa mzima wa Rukwa.

No comments: