Saturday, October 1, 2011

Naibu Waziri Lazaro Nyalandu:Serikali imepiga Marufuku Uvushaji wa Sukari Kwenda sehemu Yoyote nje ya Nchi,Serikali Pia imepiga Marufuku Uingizaji wa Bidhaa Zozote Hafifu,Mifuko ya Plastiki,Silaha na Dawa za Kulevya,



Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh Lazaro Nyalandu( Wa Sita Kulia)akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka mbali mbali za serikali katika vituo vya mipakani
---



Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh Lazaro Nyalandu, awetaka wafanyakazi wa Mamlaka mbali mbali za serikali katika vituo vya mipakani kuhakikisha kuwa, hakuna biashara yoyote ya magendo inayopenya katika mipaka hiyo.


Akizungumza na watendaji wa Mamlaka hizo katika ziara yake ya kukagua masoko na vituo vya biashara mipakani katika Eneo la Horohoro ambalo ni mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Mkoani Tanga, Mh Nyalandu amesema, biashara za magendo zinainyima serikali mapato mengi na kuneemesha watu wachache hali ambayo haikubaliki na lazima ikomeshwe mara moja.

“Serikali imepiga marufuku uvushaji wa sukari kwenda sehemu yoyote nje ya nchi, serikali pia imepiga marufuku uingizaji wa bidhaa zozote hafifu, mifuko ya plastiki, silaha na dawa za kulevya, ndio maana Mamlaka zote za udhibiti zipo katika vituo vyote vya mipakani, ninawakumbusha wajibu wenu na kuwasihi muwe wazalendo, muipiganie nchi yenu kwa kuhakikisha kuwa wadau wenu wote wanazingatia sheria.”

Kwa upande wake Mkuu wa kituo cha forodha cha Horohoro Bw Paul Kamukulu, amemuomba Naibu Waziri kusaidia kutatua kero zinazowakwaza watendaji wa serikali katika mpaka huo hali inayofanya utendaji wao wa kazi kuwa mgumu.


“Mh Waziri hali ya maisha katika eneo hili ni ngumu sana, hatuna vifaa vya kutosha kufanya kazi zetu, eneo hili halina maji, tunanunua dumu moja la maji kwa shilingi mia nane, maji yanatoka Kenya, hatuna uhakika na usalama wake, nyumba za wafanyakazi ni chache. Pamoja na yote hayo, bado tunajitahidi kwa uwezo wetu wote na kuikusanyia nchi wastani wa shilingi bilion i mbili kwa mwaka, tunaomba tusaidiwe”.


Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri Nyalandu ameahidi kufikisha kilio hicho kwa mamlaka husika ili kwa pamoja zishirikiane kutatua kero hizo na kuwawezesha watendaji hao kutimiza wajibu wao kikamilifu.


Ziara ya Mh Nyalandu kutembelea masoko na vituo vya biashara mipakani ilianzia katika Mpaka wa Tanzania na Kenya katika Mji wa Namanga Mkoani Arusha, ikaendelea katika vituo vya Himo na Holili Mkoani Kilimanjaro, na kituo cha Horohoro Mkoabni Tanga.

Pamoja na kukagua na kuhamasisha shughuli za biashara katika masoko na vituo vya biashara mipakani, ziara hizi ni mwendelezo wa utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Mh Mizengo Pinda aliewataka viongozi na Mamlaka zote za ulinzi na Usalama nchini kuhakikisha kuwa, sukari na bidhaa nyingine zozote zilipopigwa marufuku kutoka na kuingia nchini hazivuki mipaka yetu.

No comments: