Saturday, October 8, 2011

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MATUMIZI YA NJIA ZA UZAZI WA MPANGO NA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI (VVU)

JAMHURI YA MUUNGANO TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MATUMIZI YA NJIA ZA UZAZI WA MPANGO NA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI (VVU).

Tarehe 5 Oktoba, 2011, gazeti la “The citizen” lilitoa taarifa kuhusu utafiti ulioelezea kuwa, matumizi ya njia za uzazi wa mpango zenye vichocheo “hormonal contraceptives”, hususan njia ya sindano, inaweza kusababisha wanawake wanaotumia dawa hizo kuwa katika hali ambayo inarahisisha kupata maambukizi ya VVU, na pia kuwa rahisi zaidi kumuambukiza mwenzi wake iwapo mwanamke ana uambukizo wa VVU.


Kwakuwa ni matokeo ya utafiti mmoja, ambao umefuatilia watu 13 waliopata uambukizo wa VVU, na ambao walikuwa wanatumia njia za Uzazi wa Mpango (kumi walitumia sindano,na watatu (vidonge). Wizara na Shirika la Afya Duniani-ofisi ya Dar es Salaam na Makao Makuu,na wadau mbalimbali inathibitisha na kuhakiki matumizi ya njia mbalimbali za uzazi wa mpango, kwa wanawake na wanaume wenye hali au matatizo mbalimbali ya kiafya, kwamba njia zote zinazotumika ni salama na haziathiri au kusababisha matatizo ya kiafya. Kwa hapa nchini dawa zote zinatolewa kwa kufuata miongozo ambayo imeandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani.

Miongozo hiyo inabainisha kwamba, kwa mama mwenye uambukizo wa VVU haizuiliki yeye kutumia njia ya sindano ya Uzazi wa Mpango. Shirika la Afya Duniani na Serikali ya Tanzania tunafuatilia tafiti mbalimbali zinazofanywa ili kuhakikisha kuwa, miongozo wanayotoa inajumuisha mambo mapya yanayotokana na utafiti, ili matokeo yahakikiwe, kabla ya kutoa miongozo mipya.


Hata hivyo, kufuatia utafiti uliotangazwa, pia wakati njia hizi zinaendelea kuchunguzwa, Wizara inatoa maelekezo ya kuendelea kutumika kwa kondom, ili kuhakikisha kuwa kinga inaendelea na imeimarishwa.


Wizara na Shirika la Afya Duniani, tutaendelea kufuatilia suala hili na pia tafiti za kina zitafanyika, ili kubaini ukweli kuhusu suala hili. Baada ya kupata taarifa zote, wadau na wataalam kutoka sehemu mbalimbali Duniani watakutanishwa hapo mwezi wa pili mwakani na Shirika la Afya Duniani, ili kujadili tafiti mbalimbali katika eneo hili, na mapendekezo yatatolewa kuhusu matumizi ya njia za uzazi wa mpango, katika nchi zenye kiwango kikubwa cha ugonjwa wa UKIMWI (High HIV burden countries).


Uzazi wa mpango ni njia muhimu sana katika kuhakikisha kuwa, afya na ustawi kwa mtu mmoja mmoja, familia, jamii na taifa, vinalindwa na kuimarishwa. Kwa kuwa huduma hii ni muhimu, sera ya Serikali ni kutoa huduma za uzazi wa mpango bila malipo. Wizara itaendeleza huduma hizi katika ngazi zote, na kuendelea kuhakikisha upatikanaji wa njia zote za kisasa za uzazi wa mpango. Hii ni pamoja na vipandikizi, sindano, kitanzi, vidonge na kondomu.


Utafiti uliofanyika (Tanzania, Demographic & Health Survey – TDHS, 2010) umeonyesha kuwa, idadi ya watumiaji wa njia za kisasa za Uzazi, imeongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2005, hadi asilimia 27, mwaka 2010.

Lengo ni kufikia asilimia 60, ifikapo mwaka 2015. Iwapo asilimia kubwa ya wanawake wakishirikiana na wanaume watatumia njia za uzazi wa mpango juhudi hizo zitachangia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 20 hadi 30, na pia italinda afya ya watoto na kupunguza vifo vyao.


Ninapenda kuchukua nafasi hii, kuwahakikishia wananchi na kusisitiza kuwa,waendelee kutumia huduma za uzazi wa mpango, ili hatua zilizokwishafikiwa zisipungue. Aidha, matumizi ya kondomu yaendelee ili kukinga dhidi ya maambukizi mapya ya VVU. Njia nyingine zote za uzazi wa mpango, haziwezi kukinga uambukizi wa VVU, hivyo hakikisha kuwa, wakati unatumia njia nyingine kwa ajili ya uzazi wa mpango, pia tumia kondomu kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya VVU (Dual protection).


Wizara itaendela kufuatilia kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani, na wananchi watajulishwa iwapo italazimika kuwe na mabadiliko ya matumizi ya njia yoyote ya Uzazi wa Mpango, yatahitajika kufanywa. Kwa sasa ni muhimu kuendelea kutumia njia zote za Uzazi wa Mpango, ikiwemo sindano kama ilivyokuwa hapo awali.

Blandina S. J. Nyoni
KATIBU MKUU
7/10/2011

No comments: