Sunday, October 30, 2011

WAZIRI MKUU ACHANGISHA SH. MILIONI 111.6 KATIKA SADAKA YA MAVUNO OYSTERBAY

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akionyesha simu ya Bw. Leonard Kapinga (kulia) ambayea liitoa ili inadiwe katika harambee ya siku ya mavunokwenye kanisa la Mtakatifu Petro Mjini Dar es salaam Oktoba 30, 2011.Simu hiyo iligombolewa na waliohudhuria kwenye harambee hiyo na kurudishwa kwa mwenyewe gharama ya sh. 522,000/. Kushoto ni Paroko wa Kanisa la Mtakatifu Petro,Padri Joseph Mosha. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Simu ya Nokia yakombolewa kwa sh. 522,000/-

SIMU ya Nokia aina ya NOKIA 2600 ya Bw. Leonard Kapinga (37) mkazi wa Msasani leo mchana (Jumapili, Oktoba 30, 2011) ambayo kwa kawaida huuzwa kwa sh. 60,000/-hadi 65,000/- ilikuwa kivutio cha pekee katika michango ya mavuno kwa jimbo katika parokia ya Mt. Petro jijini Dar es Salaam ambapo ilichangiwa sh. 522,000/- ili ikombolewe kwa sababu mwenye nayo hakuwa na fedha za kuchagia harambee hiyo.

Bw. Kapinga ambaye hajui thamani ya simu yake kwa sababu alipewa zawadi na mama mmoja ambaye ni muumini mwenzake, alifikia hatua hiyo baada ya kuguswa na mahubiri kuhusu kumtolea Mungu sadaka ambayo inaumiza moyo wa muumini. Aliamua kutoa laini ya simu (simcard) na kumkabidhi Waziri Mkuu kama mchango wake lakini Waziri Mkuu akaamua kuwaomba watu wamchangie ili Kapinga arudishiwe simu yake.

Ibada ya mavuno kwa Kanisa la Mt. Petro lililoko Oysterbay jijini Dar es Salaam, ilifanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mbuyuni na kufuatiwa na harambee hiyo ambayo ilichangisha jumla ya sh. milioni 111. 65 zikiwa ni fedha taslimu na ahadi. Lengo lilikuwa ni kufikisha sh. milioni 100/-.

Akiwashukuru wote waliojitolea, Waziri mkuu alisema ameguswa na moyo wa kijana Leonard kwa sababu ametoa kama ambavo mafundisho ya leo yalihimiza. Vilevile alisema ameguswa na wazee wastaafu ambao wamejitokeza kwa wingi na kuchangia kila mmoja kwa kiasi chake. Wengi waliofika ni Majaji wastaafu, maafisa wa Serikali wastaafu na watumishi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Wote mliotoa michango Mungu awabariki, kijana mwenye simu iliyokusanya sh. 522,000/- ametusaidia sana, sababu mchango tumepata na simu yake amebaki nayo… wazee wangu wastaafu mmenitia moyo kwamba kustaafu siyo kwisha… mmejitoa mno na Mungu awabariki,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi waendelee kusisitiza umuhimu wa maadili ya kiroho na kimwili. “Hivi ni kwa nini mtu umuue mlemavu wa ngozi kwa kisingizio kuwa kiungo cha mwili wake kitakuongezea utajiri? Yule ni mwanadamu kama wewe, ana haki ya kuishi kama ilivyo kwa sisi wengine,” alisisitiza.

Alionya kuhusu mauaji hayo ambayo yameibuka upya na katika mwezi huu tayari watoto wawili wamekatwa viungo vyao. Alisema mwaka 2008, watu 42 wenye ulemavu wa ngozi waliuawa kutokana na imani hizo potofu.

Waziri Mkuu pia alionya Watanzania kuenzi amani iliyopo nchini kwani yanayoendelea katika nchi za jirani yanatisha na si ya kuomba yatokee kwa Watanzania. “Tuangalie yanayotokea Libya, si mambo mazuri hata kidogo. Mimi ni miongoni mwa watu wanaoamini kuwa kifo cha Gaddafi si sahihi hata kidogo, ni bora angekamatwa akashtakiwa kuliko watu kujiamulia kutoa roho ya mtu mwingine hivihivi. Watanzania tuombeane tusifike huko,” alisisitiza.

Mapema, akitoa mahubiri katika ibada hiyo, Padre Paul Haule aliwaonya waumini kuacha tabia ya kumpa Mungu mabaki au sadaka zenye ulemavu na kuwataka watoe kwa moyo wote ili Mungu azidi kuwabariki.
Akifafanua somo kutoka Kitabu cha Malaki sura ya tatu, Padre Haule alisema Mungu hapendi masazo, anataka kupewa kilicho bora na ndiyo maana aliwauliza wana wa Israeli: “Mnaninyima hata kilicho changu?”

Alisema ukombozi wa wanadamu uliofanywa na Bwana Yesu pale msalabani haukuwa wa lelemama bali ilikuwa ni sadaka ngumu iliyokuwa na uchungu. “Sadaka lazima ikuume mwamini na hata Bwana Yesu alilia pale msalabani sababu ya maumivu”.

Akifafanua kuhusu matumizi ya sadaka ya Injili, Padre Haule alisema inatumiwa kusomesha wanafunzi 43 wanaosoma katika Seminari Kuu za hapa nchini na pia kueneza Injili vijijini.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mavuno, Dk. Adelhem Meru alisema Parokia hiyo imekwishakusanya sh. milioni 37.4/- kutoka kwa waamini na katika kanda tisa za Parokia hiyo.

No comments: