Umati wa Wananchi waliofika kushuhudia tukio hilo wakiwa wamemshikilia dada wa marehemu aliyekuwa akilia huku akimlaumu marehemu kaka yake kwa kujihisisha na uchawi na kukataa ushauri wake.
Na Francis Godwin Blog,Iringa.
MTU MMOJA aitwaye Laurance Nkwera 60 mkazi wa Kijiji cha Ibani Ludewa katika Mkoa mpya wa Njombe amekufa kwa kuchomwa moto na kuungua vibaya kwa imani za kishirikina, huku nyumba yake ikiteketea, na familia yake kunusulika kifo kwa kutoboa nyumba.
Mwandishi wa mtandao huu kutoka Ludewa Basil Makungu anaripoti kuwa tukio hilo limetokea siku za hivi karibuni baada ya mlango wa Nyumba yake kufungwa nje na watu wasiojulika kutokana na mvutano uliotokea kati yake na wauaji kabla ya wauaji hao kumzidi nguvu na hatimaye kuchoma nyumba yake.
Akizungumza katika eneo la tukio Cesilia Haule ambaye ni mke wa marehemu Laurance alisema kuwa yeye na mumewe walikuwa wamelala chumbani na watoto wao wawili wakiwa wamelala sebuleni na kwamba ilipofika saa nane za usiku watu wasiojulikana waligonga mlango na kutoa masharti ya kutokutoka nje.
Ester Nkwera ni mtoto wa marehemu na Mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Kimbila anasema yeye alikuwemo ndani wakati Nyumba ikiunguzwa moto na kwamba yeye na mama yake walifanikiwa kujiokoa kwa kutoboa nyumba yao ya miti lakini Baba yake alibaki pamoja na mdogo wake Laurance.
Laurance ni mtoto wa marehemu mwenye miaka mitano tu, yeye alinusurika kifo kwa kupita katika mikono ya wauaji ambao walikuwa wamezingira nyumba hiyo ya miti huku wakiwa wamesimama pembeni kuhakikisha Nyumba na vyote vilivyomo vinateketea.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Ibani Philipo Haule, Afisa Mtendaji Kata Onesmo Haule wamesema kuwa marehemu pamoja na watu wengine wanne ni muda mrefu walikuwa wakituhumiwa kujihusisha na kuwatesa watu kwa uchawi ikiwemo kubaka wake za watu kiuchawi, kuua watu na kuwafanyisha kazi usiku kwa uchawi.
Wakizungumza kwa masharti ya kutoandika majina kwa kuhofia usalama wao wakazi wa kitongoji cha Ibani Ludewa walisema wamechoshwa na udhalilishwaji unaofanywa na wachawi ikiwemo kuwabaka wake zao kiuchawi,kuwauwa na kuwatumikisha kazi usiku na kwamba watahakikisha wanaikomesha tabia hiyo kwa kila anayehusika kwa kuwa wanafahamika.
Aidha Monica Mchiro Diwani wa Kata ya Ludewa alikiri kufanyika kwa mkutano wa hadhara octoba 11 mwaka huu unaowahusu watu watano wanaotuhumiwa na Wananchi kuwatesa kwa nguvu za uchawi hata hivyo watuhumiwa akiwemo marehemu walikana kuhusika na matukio hayo.
Bi Monica aliwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watoe taarifa polisi na ofisi za vijiji na Kata kuhusu uhalifu wowote unaotokea katika maeneo yao.
Kufuatia tukio hilo,Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Bi Georgina Bundala amemwagiza mkuu wa polisi wilaya kuhakikisha wale wote waliohusika na ukatili huo wanakamatwa haraka na kupelekwa mahakamani ili sheria iweze kufuata mkondo wake.
Aidha Bundala amekemea vikali tabia hiyo na kusema kuwa kwa jamii iliyoelimika haiwezi kufanya mambo kama hayo, na kuongeza kuwa kuna haja ya kutoa elimu kwa wananchi ili kuwajengea uelewa namna ya kukabiliana na matukio kama hayo kwa kufuata sheria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Kamishna Msaidizi wa polisi Evarist Mangala alikiri kutokea kwa mauaji hayo na kwamba taarifa kamili atatoa baada ya kupata taarifa kamili ingawa alikiri kuwa chanzo cha
mauaji ni imani za kishirikina.
Mtandao huu unalaani kwa nguvu zote kitendo hicho cha wananchi wa Ibani Ludewa kujichukulia sheria mkononi hata kuamua kupoteza maisha ya mzee Nkwera eti kwa imani za kishirikina,ni vema wananchi kuacha kufanya maamuzi mazito kama haya kwa wazee wetu kwani inapendeza kuona wananchi wanatumia vyombo vya sheria zaidi katika kuondoa tafauti zao badala ya kujigeuza wao ni Mahakama
No comments:
Post a Comment