Tuesday, November 1, 2011

Hukumu kesi ya Jerry Muro mwisho wa mwezi

Hatma ya kesi ya kula njama wala kuomba rushwa ya Sh. milioni 10, pamoja na kujifanya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Murro (30) na wenzake itajulikana Novemba 30, mwaka huu kama washtakiwa wataachiwa huru ama kwenda jela.
Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Frank Moshi ambapo aliyesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na kusema kuwa hukumu ya kesi hiyo itasomwa Novemba 30, mwaka huu mahakamani hapo.
“Kesi hii ilipangwa kutajwa leo, lakini mahakama hii inasema itasoma hukumu dhidi ya washtakiwa mwisho wa mwezi ujao,” alisema Hakimu Moshi.
Mbali na Muro, washtakiwa wengine ni, Edmund Kapama maarufu kama Dokta na Deogratias Mgasa ama Mussa.

Awali, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Januari 28, mwaka huu jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote na wengine ambao hawapo mahakamani kwa pamoja wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa la kuomba rushwa .
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Januari 29, mwaka huu katika Hoteli ya Sea Cliff, jijini walitenda kosa la kuomba rushwa ya Sh. 10,000,000 kutoka kwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa waliomba rushwa hiyo baada ya kumtishia Wage kwamba habari zake za ubadhilifu wa fedha za umma kama mhasibu wa halmashauri hiyo zitatangazwa kwenye luninga.
Katika shitaka la tatu, ilidaiwa kuwa Januari 29, mwaka huu katika hoteli ya Sea Cliff, mshtakiwa wa pili na wa tatu wakiwa na nia ovu walijitambulisha kwa Wage kwamba ni watumishi wa umma na maofisa wa Takukuru huku wakijua sio kweli.
Washtakiwa wote kwa nyakati tofauti walikana mashitaka yao na wako nje kwa dhamana.
CHANZO: NIPASHE

No comments: