Friday, November 11, 2011

MBUNGE WA MBARALI AHUKUMIWA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mbeya, imemtia hatiani Mbunge wa Mbarali, Modestus Dickson Kilufi kwa kosa la kutishia kuua kwa maneno kwa kukusudia na kumuhukumu kwenda Jela miezi 10 au kulipa faini ya shilingi 500,000.

Mwandishi wa mtandao huu kutoka Mbeya Moses Ng'wat anaripoti kuwa hukumu hiyo ilitolewa leo na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Michael Mtaite ambaye alikuwa akisikiliza shauri hilo, ambalo Kilufi alishtakiwa alidaiwa kutishia kwa maneno kumuua Afisa Mtendaji wa Kata ya Ruwiwa wilayani Mbarali, Jordan Masweve.

Katika hukumu hiyo iliyosomwa kwa takribani saa moja, Hakimu Mtaite alisema Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka na hivyo inamtia hatiani Mshtakiwa.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo, Hakimu Mtaite alitoa nafasi kwa mawakili wa pande zote mbili kutoa mapendekezo yao na ndipo Wakili wa Serikali, Epimark Maborouk alipoiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili liwe fundisho kwa watu wengine wasifanye kosa hilo.

Kwa upande wa Wakili wa utetezi, Edson Mbogoro alisema kuwa kwa hata upande wa Serikali unakiri kuwa mteja wake hana rekodi ya kufanya uhalifu,kwa kuwa ameoa, ana familia inayomtegemea na ni Mbunge anayewakilisha watu wengi, anapingana na hoja za wakili wa Serikali na badala yake anaiomba mahakama impunguzie adhabu.

Alisema pia kwa kuwa mahakama ina wigo mpana wa kumuadhibu mshitakiwa, ni vema ikamtafutia adhabu nyingine badala ya kifungo cha gerezani.

Hata hivyo kabla ya kumaliza kutoa mapendekezo yake, Wakili wa Serikali Maborouk aliingilia kati na kupinga hoja ya wakili wa utetezi ya kutaka kuielekeza mahakama namna ya kumuadhibu mshtakiwa kwa madai kuwa nafasi aliyopewa ni ya kutoa sababu za kumsaidia mshitakiwa kupunguziwa adhabu na sio kuielekeza mahakama namna ya kutoa hukumu.

Hakimu Mtaite alikubaliana na Wakili wa Serikali na kumtaka Wakili wa Utetezi, Maborouk kutoa sababu za kuishawishi mahakama impunguzie mteja wake adhabu na sio vinginevyo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili ndipo Hakimu Mtaite alipotoa hukumu hiyo kwa Mbunge Kilufi ya kwenda Jela miezi 10 kama hatoweza kulipa faini ya shilingi 500,000.

Mheshimiwa Kilufi alitolewa ndani ya Chumba cha Mahakama chini ya ulinzi mkali wa Polisi na kuingizwa katika chumba cha makalani wa Mahakama, ambako alilipa faini hiyo na kuachiwa huru.

Ijumaa Oktoba 6, mwaka huu Kilufi alikamatwa na Polisi akiwa ofisini kwake na kusafirishwa chini ya ulinzi mkali kwenda Jijini Mbeya, ambako alilala mahabusu na kuachiwa kwa dhamana kesho yake kabla ya kupandishwa kizimbani Oktoba 10, mwaka huu na kusomewa mashtaka yake ambayo aliyakana na kurudishwa rumande wakati mahakama ikifikiria masharti ya dhamana.

Mbunge huyo alisota rumande kwa siku tatu kabla ya kupewa dhamana na ndipo kesi yake ilipoanza kuunguruma mahakamani hapo na kufikia mwisho jana kwa mshtakiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa.

Katika kesi ya msingi, Kilufi (51), alishtakiwa kwa kusa la kutishia kuua, kosa alilolifanya Marchi 16, mwaka huu akiwa katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.

Akimsomea mashtaka yake mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Griffin Mwakapeje alisema Mtuhumiwa Kilufi alitenda kosa hilo March 16, 2011 mwaka huu akiwa wilayani Mbalali, ambako alitishia kumdhuru Jordan Masweve.

Alisema kitendo kilichofanywa nna mtuhumiwa siku hiyo ni kinyume cha kifungu cha 89, kifungu kidogo cha 2 (a) cha sheria ya kanuni ya adhabu, sura ya 16, kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Chanzo Blog ya Francis Godwin

No comments: