Napenda kuwajulisha kwamba Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imepokea taarifa za ripoti za ukaguzi wa vyama vya siasa zilizowasilishwa kwangu na Mhe. John B. Tendwa ambaye ni Msajili wa vyama vya Siasa, tarehe 20 Agosti 2011 zikiwa zimekwisha kaguliwa na kampuni binafsi za ukaguzi. Ninapenda kuvipongeza vyama vyote vilivyowasilisha taarifa zao za ukaguzi
Taarifa hizi ninazozitoa leo ni matokeo ya ukaguzi wa taarifa za fedha za vyama vya siasa uliofanywa na kampuni binafsi za ukaguzi kwa kipindi cha miaka tofauti kama zilivyowasilishwa kwangu.
- MUHTASARI WA UKAGUZI WA VYAMA VYA SIASA VILIVYOWASILISHA RIPOTI ZA UKAGUZI
- Matokeo ya Ukaguzi
- Hadi ninapowasilisha taarifa hii kwenu, ni vyama vitano (5) tu ndio vilivyoweza kuwasilisha hesabu zilizokaguliwa kwa miaka tofauti tofauti.
- Hesabu zilizowasilishwa ni
- Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2008 - TAC
- Chama cha Wananchi (CUF) kwa mwaka 2009 – IMARA CONSULTANTS
- Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kwa mwaka 2009 – SHEBRILA & CO.Chama cha NCCR Mageuzi kwa mwaka 2010 – RELIABLE CONSULTANTS
- Chama cha UDP kwa mwaka 2007 – PHILIP & CO.
Katika kaguzi hizo matokeo yameonesha kuwa vyama vyote vilivyokaguliwa vimepata hati inayoridhisha.
Nimepitia na kubaini kuwa hesabu hizo zimekaguliwa na Wakaguzi ninaowatambua na wanaotambulika na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA). Kwa kuwa vyama vilivyowasilisha hesabu hizo vilikaguliwa na Wakaguzi wanaotambulika, ni wazi kuwa Wakaguzi waliokagua hesabu hizo walikuwa na sifa za kufanya ukaguzi huo. Hata hivyo, hesabu hizi hazikuwasilishwa kwa wakati unaotakiwa kisheria.
Ninapenda, kukumbusha kuwa kifungu cha 14(1) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya mwaka 1992 kama ilivyofanyiwa mabadiliko na Sheria Na. 7 ya mwaka 2009, kinavitaka vyama vyote vilivyo na usajili wa kudumu kuwasilisha kila mwaka kwa msajili wa vyama vya hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Kwa mantiki hiyo basi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ndiye mwenye wajibu wa kukagua hesabu za vyama vya siasa.
Kwa mujibu wa Sheria hii, Vyama vya Siasa vinapaswa kuwasilisha hesabu zao ambazo hazijakaguliwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya Ukaguzi. Kwa sasa hesabu zilizowasilishwa kwangu zimekwisha kaguliwa na Kampuni binafsi za ukaguzi.
Baada ya kuchambua kwa makini ripoti hizo, imeonekana dhahiri kwamba haitakuwa vema nikae kimya bila kutoa maelezo kwa Umma kwani utaratibu uliotumika wa kuwasilisha hesabu zilizokwisha kaguliwa na kampuni binafsi za ukaguzi si sahihi na zinakiuka taratibu.
Ili kudumisha uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za umma tunapenda kuufahamisha umma wa watanzania kuwa Ofisi hii iko makini na itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 kama ilivyofanyiwa mabadiliko na Sheria Na.7 ya mwaka 2009. Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi itaendelea kuhimiza vyama vya siasa kuwasilisha hesabu zao kwa lengo la kuhakikisha mapato na matumizi yanafanyika kwa manufaa ya umma na kama ilivyokusudiwa.
- MUHTASARI WA UKAGUZI WA VYAMA VYA SIASA NA WAGOMBEA WALIOSHIRIKI KATIKA UCHAGUZI MKUU ULIOFANYIKA TAREHE 31 OKTOBA 2010
Kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 kifungu Na. 19 (4) inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa hesabu za vyama vya siasa na wagombea walioshiriki katika uchaguzi.
Hesabu za vyama vya siasa zilizowasilishwa kwangu ni za vyama vitano (5) tu kwa ajili ya maandalizi ya awali ya ukaguzi kufanyika. Vyama hivyo ni kama vifuatavyo:
(i) Chama cha CCM
(ii) Chama cha CHADEMA
(iii) Chama cha CUF
(iv) Chama cha JAHAZI ASILIA
(v) Chama cha TLP
Kifungu cha 19 (4) cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 kinaeleza kuwa, “Kumbukumbu zote za gharama za uchaguzi zitakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa”
Kifungu cha 20 (1) cha Sheria hii kinasema, “Chama cha Siasa na kila mgombea ambaye anatakiwa kwa masharti ya sheria kutoa taarifa ya kiasi na chanzo cha fedha kinachotarajiwa kutumika kama gharama za uchaguzi akishindwa kutoa taarifa ya fedha hizo, bila ya kuwa na maelezo yanayoridhisha, chama au mgombea atapoteza sifa na hatoweza kushiriki katika uchaguzi”.
Kwa maelezo hayo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anapenda kuvijulisha vyama vyote vya siasa na wagombea wote walioshiriki katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 31 Oktoba 2010 kuwa kisheria ni kosa kutowasilisha au kuchelewa kuwasilisha hesabu kulinagana na kifungu cha 19 (4) na kifungu cha 20 (1) kinavyoagiza.
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali inawahimiza wagombea wote na vyama vya siasa kuzingatia Sheria kwa ajili ya maslahi ya umma katika kudhibiti matumizi mabaya na kuepuka vitendo vinavyokatazwa.
Imetolewa na,
Ludovick S. L. Utouh
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
No comments:
Post a Comment