kufuatia kuwepo na mwamko mdogo unaondelea kwa kasi kwa baadhi ya wazazi katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa umekuwa ukichochea watoto wengi wa kike katika shule za sekondari kuacha masomo baada ya kupata ujauzito huku wazazi wao wakifurahia kuondokana na kero ya kuwasomesha watoto wao.
Mwandishi wa mtandao huu kutoka Sumbawanga Elizabeth Ntambala anaripoti kuwa ,Hayo yameelezwa na baraza la Madiwani wa Manispaa, katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa hivi karibuni wakati wakijadili mambo ya maendeleo .
Diwani wa kata ya Mazwi Joseph Ngua alisema wazazi wengi wasio na mwamko wa kielimu wamekuwa wakifurahia vitendo vya mimba kwa watoto na mara nyingi wanapoonekana wamepewa mimba wamekuwa wakishirikiana na wanaume wanao wapa ujauzito ili kuficha siri.
Katika taarifa yake Afisa Elimu sekondari Mohamed Nanyanje alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano wanafunzi 202 wa shule sita za sekondari katika Manispaa ya Sumbawanga wameshindwa kuendelea na masomo yao baada ya kupata ujauzito.
Nanyanje alizitaja shule hizo na idadi ya wanafunzi hao kwenye mabano kuwa ni Mtipe (43) Kizwite (26),Mbizi (25), Kalangasa (16) Itwelele.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Mkurugenzi Silyvia Siriwa alisema kuwa tatizo la mimba mashuleni linaweza kupungua iwapo wazazi wenyewe watakerekwa na tatizo hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola pale wahusika wanaotenda makosa hayo wanapotiwa mikononi mwa sheria.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Sabas Katepa alisema ipo haja kwa halmashauri hiyo kutengeneza sheria ndogo ambayo itawabana wanafunzi wa kike na wanaume wanawapa ujauzito kwa kuwakamata na wote kwa pamoja kushtakiwa kwa kosa hilo.
“Kwa namna moja au nyingine hao mabinti wanapata kichwa kwasababu hawaghasiwi na vyombo vya dola na ndio maana hata wanashindwa kutoa ushirikiano pale wanapohitajika kufanya hivyo, kwa hiyo hii itawashtua wao na wazazi pia.” Alisema Katepa.
Habari na Francis Godwin
No comments:
Post a Comment