Wednesday, December 28, 2011

John Mnyika:Serikali itake Israel Waombe Radhi;Tukijiheshimu,Tutaheshimiwa





Mbunge wa Ubungo-Chadema,Mheshimiwa John Mnyika


---


Kurugenzi
ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inaitaka
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa tamko juu ya kauli ya
Waziri wa Ulinzi wa Israel ya kwamba nchi yetu si ya muhimu wala ya
maana.





Waziri
Barak alifanya mahojiano na Radio Israel na kutoa kauli ambayo
imenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari vya nchi hiyo wiki iliyopita
kuwa “ Germany, France and England are not Tanzania, Mauritania or
Tripolitania…..these are very important, very relevant countries and we
don’t have an interest in increasing tensions with them or making them
bitter enemies”.



Kwa
kauli hii serikali ya Israel inaiona Tanzania sio nchi ya muhimu wala
ya maana hata kufikia hatua ya kuilinganisha na eneo tu ndani ya Libya
linaloitwa Tripolitania.



Tunamtaka
Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa, Benard Membe kuitaka
serikali ya Israel kuomba radhi kufuatia kauli hiyo au kueleza wazi
iwapo mazungumzo hayo ya Waziri Barak ni msimamo wa nchi hiyo kuhusu
uhusiano wa kidiplomasia wa mataifa yetu.



Barua
pekee ya balozi wa heshima wa Tanzania nchini Israel, Kasbian Nuriel
Chirich kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Avigdor Lieberman ya
kulaani matamshi hayo ya Waziri Barak na kumkaribisha mwakilishi wa
Israel kutembelea Tanzania haitoshi kuifanya serikali ya nchi hiyo
kutambua athari za kidiplomasia za kauli iliyotolewa.


Aidha
kwa kuwa serikali imekuwa ikieleza kwamba Tanzania ina mahusiano mazuri
ya kiulinzi na Israel, ni muhimu pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Dr Hussein Mwinyi akaeleza umma iwapo kauli hiyo ya
Waziri Barak ndio msingi wa mahusiano yaliyopo kati ya nchi zetu kuhusu
ulinzi na usalama.



Kurugenzi
ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa inachukua fursa hii kurudia
kuwakumbusha watanzania kwamba kupuuzwa huku kwa nchi yetu katika medani
ya kimataifa kunatokana na sera mbovu ya mambo ya nje chini ya utawala
wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).



Tanzania
imepoteza heshima katika siasa za dunia kutokana na diplomasia yetu
kujikita katika kuomba omba kimataifa; pamoja na kuwa kimaneno na
maandishi serikali inazungumza kuhusu diplomasia ya kiuchumi, kivitendo
mahusiano yetu yamejengeka katika misingi ya utegemezi, kupungua kwa
urari wa kibiashara na kuachia mianya ya uporwaji wa rasilimali.



Kurugenzi
ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa inatambua kwamba wakati wa
uongozi wa awamu ya kwanza wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania
ilikuwa na heshima na sauti kimataifa sio tu katika jitihada za
ukombozi kusini mwa Afrika bali pia katika mahusiano ya kisiasa,
kiuchumi na kijamii baina ya nchi za kusini na mataifa mengine duniani.



Hali
ya Tanzania kupoteza sauti katika medani ya kimataifa imedhihirika pia
hivi karibuni katika mkutano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi (COP 17)
uliomalizika hivi karibuni nchini Afrika Kusini; wakati nchi yetu ikiwa
ni miongoni mwa waathirika wakubwa zaidi wa mabadiliko ya tabia nchi.
Iwapo hatua hazitachukuliwa kurejesha heshima na sauti ya Tanzania
kimataifa maamuzi mengi yatafanyika yenye athari kwa wananchi wengi bila
ushiriki wao thabiti kama yanayoendelea hivi sasa kuhusu Mikataba ya
Kiuchumi na Nchi za Jumuia ya Ulaya (EPA) yenye madhara kwa wakulima na
wenye viwanda nchini.



Kurugenzi
ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa inatoa mwito kwa watanzania
kuendelea kuunganisha nguvu ya umma kusimamia uwajibikaji na kufanya
mabadiliko ya kimsingi ya kiuongozi, kisera na kimfumo ya kitaifa ili
kuweza kurejesha nafasi na heshima ya Tanzania kimataifa katika
mazingira ya sasa ya ushindani wa kiuchumi, kiulinzi, kijamii na
kisiasa.





Kauli
ya Waziri Barak nimuendelezo tu wa mataifa mbalimbali kuifanya Tanzania
na baadhi ya nchi nyingine za Afrika kuwa hazina heshima wala sauti
katika siasa za kimataifa kama ambavyo Serikali za Uingereza na Marekani
zimeweka masharti yenye mwelekeo wa ukoloni mamboleo kuhusu masuala ya
ushoga na usagaji.




Hatua
za kupinga kauli za kudharauliwa na kulazimishwa mambo tusiyoyataka
ziende sambamba na kudhibiti mianya yote ya ufisadi wa kimataifa,
uwekezaji uchwara na kutetereka kwa misingi wa utawala wa kisheria
masuala ambayo yanasababisha migogoro na pia rasilimali za nchi
kutokutumika kwa manufaa ya wananchi walio wengi; tukijiheshimu,
tutaheshimiwa.




Wenu katika Demokrasia na Maendeleo,



John Mnyika (Mb)



Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa (CHADEMA)

No comments: